Dar es Salaam. Baada ya kukaa nje ya utumishi kwa kipindi cha siku 412, hatimaye Albert Chalamila amerejea katika nafasi za uteuzi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.
Chalamila ameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan leo Julai 28, 2022 akichukua nafasi ya Meja Jenerali Charles Mbuge.
Hii si mara ya kwanza kwa Chalamila kutumikia wadhifa huo, kwani aliwahi kuwa mkuu wa mikoa ya Mwanza na Mbeya.
Utumishi wake katika nafasi ya mkuu wa mkoa ulikoma Juni 11, 2021 baada ya Rais Samia kutengua uteuzi wake na nafasi hiyo kujazwa na Robert Gabriel.
Kada huyo machachari wa CCM aliyewahi kuwa mwenyekiti wa chama hicho katika Mkoa wa Iringa, ndiye aliyekuwa mkuu wa mkoa wa kwanza kutenguliwa na Rais Samia tangu aingie madarakani.
Chalamila aliteuliwa kuwa mkuu wa mkoa wa Mwanza Mei 15, 2021 akitokea Mbeya alikodumu kwa takribani miaka minne tangu Julai 29, 2018 alipoteuliwa na Hayati Dk John Magufuli.
Kabla ya hapo Chalamila alikuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, wadhifa alioupata Desemba 5, 2017 baada ya kushinda katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho.
Kabla ya kuibukia katika siasa, Chalamila alikuwa mhadhiri msaidizi katika Chuo Kikuu cha Tumaini mkoani Iringa na amewahi kuwa mwalimu katika shule mbalimbali.
Kauli yake ya kuwataka wananchi kujitokeza na mabango hata yenye matusi katika ziara ya Rais Samia mkoani Mwanza ni moja ya mambo yanayotajwa kuwa sababu za kutumbuliwa kwake.
“Tuweze kumpokea Rais wetu kwa mabango mengi, mabango aina yoyote, hata kama ataandika tusi, aandike. Yoyote yale,” alisema Chalamila wakati akiwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika ziara hiyo.
Kauli hiyo ya Chalamila ilikuja siku chache baada ya Rais Samia kuonya tabia za ulipukaji kwa viongozi aliowateua.
“Nimewasimamia Ma-RC na Ma-RAS ili tuone shughuli itakavyokuwa huko, mfano pale Mwanza nimesema kiberiti na petroli kwa sababu Samike (RAS) mkimya lakini ana zake, yule mwingine RC Chalamila ni mlipukaji,” alionya.