Uajiri wa R Kelly ulishafikia thamani ya dola za Marekani 100 milioni, wastani wa Sh230 bilioni. Leo ni mufilisi. Hana kitu isipokuwa madeni.
Mapambano ya kesi za kunyanyasa watoto wadogo kingono, malipo ya talaka na malezi ya watoto kupitia kwa akina mama aliotalikiana nao, jumlisha madeni ya kodi, kwa pamoja, imekuwa sababu ya utajiri wa R Kelly kupukutika.
R Kelly alikuwa juu ya uso wa dunia kimuziki. Usingemwona kwa urahisi kwa jinsi alivyokuwa ‘busy’ katika shughuli zake za kila siku na alilindwa kwa ukaribu. Leo hana uhuru wake tena!
Miaka 30 jela inamhusu. Hatia yake ni kutumia umaarufu wake kunyanyasa watoto kingono, tena wakiwa mashabiki wake. R Kelly amekutwa na hatia ya kuvunja Sheria ya Biashara ya Ngono ya Marekani.
Hivi ndivyo maisha yanavyoweza kugeuka juu chini. Kutoka kuwa binadami unayeheshimika mpaka kuonekana hufai, hivyo kutupwa gerezani ukachangie maisha na jumuiya ya wahalifu.
Septemba mwaka jana, R Kelly alikutwa na hatia. Jumatano iliyopita (Juni 29), ilikuwa siku ya hukumu. Jaji Ann Donnelly, alisoma hukumu iliyohitimisha harakati za muda mrefu.
Awali, zilikuwepo fununu nyingi kuwa R Kelly alikuwa akiwanyanyasa wanawake wadogo kingono. Vyombo vya habari vilipuuza na polisi waliona ni uzushi.
Wanawake watatu, wote Wamarekani weusi, waliamua kukata mzizi wa fitina, walipotengeneza ‘documentary’ (makala maalumu), wakaipa jina la “Surviving R. Kelly”.
Mtayarishaji mkuu wa Surviving R. Kelly ni Dream Hampton, alisaidiana na Brie Miranda Bryant na Tamra Simmons. Hao ndio wanawake watatu, Wamarekani weusi walioamua kukata mzizi wa fitina.
Surviving R. Kelly, ilifuatiwa na kampeni ya ‘MeToo’, iliyolenga kuwahamasisha watu wengi zaidi ambao ni waathirika wa vitendo vya R Kelly, kujitokeza na kuusema ukweli.
Documentary ya Surviving R. Kelly, ilibeba simulizi za watu walioathirika kwa namna moja au nyingine na vitendo vya R Kelly. Walizungumza waathirika wenyewe mpaka wazazi wa watoto waliofanyiwa vitendo viovu na R Kelly.
Surviving R. Kelly, ikawezesha hoja zilizojenga mashtaka. R Kelly akakamatwa, akafikishwa mahakamani. Mwisho kabisa, hukumu imempitia.
Wakili wa R. Kelly, Jennifer Bonjean, alitoa ombi kwa Jaji Ann Donnelly kuwa mwanamuziki huyo alikulia kwenye mazingira ambayo alinyanyaswa kingono, hivyo apewe msamaha. Ombi hilo halikuzingatiwa.
R Kelly aliwezaje
Kumekuwa na hoja endelevu kuwa R Kelly ameonewa kwa sababu ni Mmarekani mweusi. Majibu rahisi ni kwamba waathirika wengi waliojitokeza kulalamikia vitendo vya R Kelly ni Wamarekani weusi. Je, wametumika?
Watayarishaji wa mfululizo wa documentary (docuseries) ya Surviving R. Kelly ni Wamarekani weusi. Je, na wao wanatumika?
Tuhuma za R Kelly ni za muda mrefu. Zinaingia mpaka Mahakama ya Illinois mwaka 1995, ilipolazimika kuvunja ndoa ya R Kelly na mwanamuziki mdogo wakati huo, Aaliyah. Mahakama iligundua R Kelly alimuoa Aaliyah akiwa na umri chini ya miaka 18, kinyume na sheria ya ndoa.
Ukifutilia docuseries ya Surviving R. Kelly, unapata ujumbe kuwa watoto wa kike wenyewe ndio walikuwa wakimfuatilia mwanamuziki huyo. Walijisogeza kwake kwa kuwa walimpenda kwa kazi zake, naye akawatumikisha kingono.
Lawama nyingi kwa wazazi. Walitoa uhuru mkubwa kwa watoto wao, kuwaamini bila kufuatilia, ni sababu ya watoto wao kumfikia R Kelly ambaye hakuwapokea kama viumbe wasio na hatia, aliwatumia na kuwanyanyasa.
Mfano, Aaliyah alipelekwa kwa R Kelly na mjomba wake, Barry Henkerson ambaye alikuwa prodyuza mwenzake kwenye studio za Chicago Music Company. Barry alimfahamu vizuri R Kelly, lakini alimwacha awe jirani na Aaliyah na matokeo yake yakashuhudiwa makubwa ya R Kelly kumuoa Aaliyah aliyekuwa na umri wa miaka 15.
Sparkle alifanya kazi na R Kelly tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990. Alikuwa ‘back vocalist’ wake, vile vile Sparkle aliingiza sauti kwenye nyimbo ambazo R Kelly alizitengeneza akiwa prodyuza. Hata albamu ya ‘Age Ain’t Nothing but a Number’, Sparkle amejaza sauti karibu nyimbo zote. Sparkle pia alishirikiana na R Kelly katika ‘Be Careful’, ambayo ni bonge la hit. Hivyo, Sparkle anamjua vizuri R Kelly, lakini akakubali kumkabidhi binti mdogo Reshona, ili amlee kimuziki, matokea yake, binti akatumikishwa kingono.
Jerhonda stori yake ni jinsi wazazi wake walivyokuwa wanamwamini na kumpa uhuru kupita kiasi. Alipowaambia anakwenda kwa rafiki yake, wakamkubalia bila kufuatilia, matokeo yake aliangukia kwenye mikono ya R Kelly.
Katika documentary ya BBC yenye jina, ‘Sex, Girls, STDs: R Kelly Sex Scandal’, wameguswa Lisa Van Allen, Faith Rogers, Kitti Jones, Asante McGee na Joycelyn Savage. Hapa pia nisimulie kuhusu Joycelyn alivyonasa kwa R Kelly, akanogewa na kugoma kurejea kwa wazazi wake.
Joycelyn anatamani kuwa mwanamuziki. Wazazi wa Joycelyn wapo vizuri kimaisha. Jumba la kifahari Atlanta, wanaendesha magari ya bei mbaya. Hawana njaa. Walipoona mtoto wao kipaji chake ni muziki, waliamua kumtafuta R Kelly ili amsaidie kumuingiza kwenye lebo.
Baba wa Joycelyn, Tim Savage na mama yake, Jonjelyn Savage, walipata namba ya R Kelly ambaye alikubali kumpokea binti yao. Faith Rogers alipofanikiwa kuchomoka kwenye jengo la R Kelly, aliwatafuta wazazi wa Joycelyn na kuwaeleza kinachoendelea mjengoni kuwa mtoto wao anashiriki mapenzi ya kikundi na R Kelly.
Faith aliwaambia kuwa R Kelly ana maambukizi ya magonjwa ya ngono (STDs). Na alithibitisha hivyo kwa kuwa baada ya kutoroka, alipima na kukutwa na STDs.
Baada ya hapo, wazazi wa Joycelyn walitumia jitihada nyingi kumpata binti yao bila mafanikio. Mamlaka za usalama Marekani, wakiwemo FBI, ziliingilia kati lakini Joycelyn mwenyewe akawa hataki kurudi kwa wazazi wake.
Tunarudi kule kule, wazazi wa Joycelyn walijua kila stori iliyokuwa inaendelea kuhusu R Kelly, lakini waliona uzushi, wakampeleka kwake. Mpaka leo wanaendelea na mapambano ya kumpata bila mafanikio. Mtoto kaganda kwa R Kelly.
Hukumu itamsaidia?
Nilifuatilia kesi karibu 25 za R Kelly kuwanyanyasa kimapenzi watoto wadogo. Mambo yenye kuzungumzwa ni yale yale; Mosi, R Kelly anawapiga wanawake. Mtalaka wa R Kelly, Andrea Lee, naye alilizungumza hili, kwamba ndiyo kisa cha kuomba talaka. Andrea na R Kelly waliachana mwaka 2009 wakiwa na watoto watatu.
Pili, R Kelly aliwaambukiza magonjwa ya ngono watoto. Tatu, watoto hawakuwa na hiari, kwani aliwaamrisha kuliko kuwaomba. Alipofika aliwaambia vua, geuka mbele, geuka nyuma, aliyebisha alipigwa. Nne, ilikuwa ukishaingia kwa R Kelly anahakikisha huwasiliani na ndugu zako. Tano, sheria ni kumwita R Kelly daddy, ukimwita tofauti na hapo unachezea mkong’oto.
Historia inaonyesha kuwa R Kelly alikulia kwenye nyumba ya wanawake watupu na alipokuwa mdogo alitumikishwa kimapenzi na mwanamke aliyekuwa mkubwa sana kwake. R Kelly alikuwa na rafiki wa kike aliyeitwa Lulu, waliyependana sana tangu akiwa na umri wa miaka minane. Lulu aliuawa akiwa mdogo na kumuumiza sana R Kelly. Lingine, R Kelly alipokuwa na umri wa miaka 11, alipigwa risasi ya bega. Mpaka leo risasi hiyo ipo mwilini. Je, mambo hayo hayawezi kuwa sababu ya tabia yake ya sasa?
Inakuwaje kijana aliyetoka kwenye umaskini mkubwa. Aliyelelewa na mama bila baba. Aliyeanza maisha ya muziki kwa kuimba kanisani, kisha mtaani, akiwaburudisha wasafiri wa treni za kampuni ya Chicago ‘L’, anapata mafanikio makubwa. Yupo juu ya ulimwengu. Tajiri, maarufu, anapendwa, lakini anaharibu sifa zote kwa tabia yake ya kunyanyasa wanawake hasa watoto? R Kelly anahitaji msaada.
Kama gerezani atapata msaada mzuri wa kisaikolojia, pengine R Kelly atabadilika.