Rais wa Sri Lanka, Gotabaya Rajapaksa inaelezwa kuwa anatafakari kulikimbia Taifa hilo la kisiwa kwa kutumia Boti ya doria ya Jeshi la wanamaji baada ya kutokea tofauti kati yake na Maafisa wa uhamiaji katika uwanja wa ndege ambao wamekataa kugonga muhuri passport yake.
Rajapaksa ameahidi kujiuzulu kesho na kupisha njia ya kukabidhi madaraka kwa amani kufuatia maandamano makubwa dhidi yake kuhusu mzozo mkubwa kabisa wa kiuchumi nchini humo, Maafisa wanasema Rais huyo mwenye umri wa miaka 73 alitaka kusafiri kwenda Dubai.
Akiwa rais, Rajapaksa ana kinga ya kukamatwa, na inaaminika anataka kwenda ng'ambo kabla ya kujiuzulu ili kuepusha uwezekano wa kukamatwa lakini Maafisa wa uhamiaji walikataa kwenda katika eneo la wageni mashuhuri kupiga muhuri kwenye passport yake, wakati akisisitiza kuwa hawezi kutumia maeneo ya wasafiri wa kawaida akihofia kushambuliwa.
Kaka yake mdogo, Basil Rajapaksa aliyejiuzulu kama Waziri wa Fedha mwezi Aprili, aliikosa ndege yake mapema leo kwenda Dubai baada ya mkwamo kama huo katika uwanja wa ndege.