KAMATI ya Utendaji ya Klabu ya Yanga imefanya kikao chake cha kwanza cha kikatiba jana (Jumamosi) Julai 30, 2022 kwenye Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Rais wa klabu timu hiyo, Injinia Hersi Said.
Pamoja na mambo mengi yaliyojadiliwa kwenye kikao hicho kamati ya utendaji ilipokea na kujadili pendekezo la Senzo Mazingiza la kutokuongeza mkataba wake unaoisha leo Julai 31, 2022.
Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo ilieleza Senzo aliwasilisha ombi hilo lenye muktadha wa sababu za kifamilia ambayo amekuwa nayo mbali kwa kipindi cha miaka mitatu.
Ombi hilo lilipokelewa na baada ya kujadiliwa, Kamati ya utendaji ilikubali ombi hilo na kumteua Wakili Simon Patrick kuwa Afisa Mtendaji Mkuu wa mpito (Interim Executive Officer).
Klabu hiyo imemshukuru Senzo kwa utumishi wake uliobora hasa katika mchango wake kwenye eneo la utawala na kumtakia kila la heri.
Senzo raia wa Afrika Kusini alijiunga na Yanga Agosti 31, mwaka jana na kabla ya kuteuliwa kaimu mtendaji mkuu alikuwa mshauri hasa kuelekea katika mfumo wa mabadiliko yaliyofanyika kwenye klabu hiyo.
Mbatha aliwahi kuhudumu kwenye nafasi hiyo katika klabu ya Simba kabla ya kuachana nayo na kutua Yanga alikodumu kwa miaka miwili tu.