Serikali yapewa neno ununuzi treni zilizotumika



SERIKALI ya Tanzania imeshauriwa kufikiria upya mpango wake wa kununua vifaa vya treni ya umeme vilivyotumika, maarufu kama mitumba, ili kujua kama hauna athari kwa taifa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ushauri huo ulitolewa jana Jumatatu, tarehe 4 Julai 2022, muda mfupi baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, kusema Serikali imetoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa hivyo.

Ikiwemo seti za treni 10, vichwa vya treni vipya 17, pamoja na mabehewa ya abiria 57, ambapo baadhi yake vitakuwa vilivyotumika lakini vyenye hali nzuri.

Akizungumza na MwanaHALISI Online kwa njia ya simu, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi, ameishauri Serikali iangalie upya uamuzi huo kwani una athari ikiwemo kufungua milango ya rushwa na udanganyifu.


 

Rais Samia Suluhu Hassan
“Ninavyofahamu kama Serikali hairuhusu kununua magari chakavu, sioni kwa nini wanunue hizo treni chakavu. Hizo chakavu unaweza danganywa kilomita zilizotembea kumbe sio. Ule udanganyifu, mambo ya rushwa zitaingia. Waangalie upya shughuli za manunuzi. Sheria za vyombo vya moto hairuhusu kununua vyombo chakavu. Wasinunue na wakinunua itakuwa suala la rushwa,” amesema Prof. Moshi na kuongeza:

“Mtu anaweza kudanganya bei fulani kumbe siyo. Tunanunua tunaambiwa yametembea kilomita 50,000 kumbe imetembea kilomita 200,000. Hatuna sababu ya kukwepa kununua kipya sababu itatupa vitu vizuri na matengenezo yake yatakuwa madogo kuliko ukichukua ya zamani na hii itaongeza gharama za matumizi ya Serikali. Wahakikishe wanazingatia sheria moja kwa moja bila kukiuka.”

Naye Msemaji wa Sekta ya Miundombinu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Mohamed Mtambo, ameishauri Serikali isitishe mpango huo, badala yake ifanye uchambuzi wa kina kujua athari zake.


“Mchakato huu lazima uangaliwe upya na kwa umakini sana kwa sababu unavyonunua hivi vitu unatuma vigezo kwa mtengenezaji, unamwambia naomba unipe jembe nakwenda kulima kwenye mawe na mtengenezaji atakupa vochwa vya treni kulingana na vigezo vyako ulivyomtumia kulingana na mazingira na hali ya hewa yako,” amesema Mtambo na kuongeza:

“Hivi used vimetengenezwa kwa vigezo vya aliyenunua awali, unaweza kuta yeye ana baridi sana, sisi tunachoshughulika nacho chuma ambacho kinatanuka na kinaathirika na joto. Hili zoezi ni hatarishi na si jambo la kuliendea harakahara bila kulifanyia uchambuzi wa kina.”

Mwanahalisi


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad