Watu wanne wamenusurika kifo mara baada ya bajaji namba MC 567 CJK aina ya TVS iliyokuwa ikitoka maeneo ya stendi kuu ya mji wa Njombe kuelekea katikati ya mji kupinduka kutokana na mlipuko mkubwa wa simu ya abiria uliosababisha moto.
RPC wa Njombe Hamis Issah amesema bajaji hiyo imepinduka kutokana na dereva kugeuka nyuma kutokana na taharuki ya kulipuka kwa simu ndogo mali ya Siston Antony katika Barabara kuu ya Njombe-Songea majira ya saa tano asubuhi.
“Moto umelipuka mkubwa na dereva wa bajaji akageuka kuangalia abiria wake na kushindwa kuiongoza akaiachia bajaji wakapinduka, baada ya ajali hiyo Polisi imeingilia kati kutokana na Mmiliki wa bajaji kutaka kulipwa na abiria ambaye ni Mmiliki wa simu iliyosababisha mlipuko na kupelekea kupinduka kwa bajaji na kuharibika”
Aidha Kamanda Issa ametoa wito kwa Wamiliki wa vyombo vya moto kuwa na bima za vyombo vyao ili kuepusha usumbufu kama huo huku pia akitoa rai kwa Wamiliki wa simu kuwa makini na matumizi ya simu zao na kusema abiria wote walipelekwa Hospitali kwa ajili ya matibabu ya majeraha madogo na kuruhusiwa kutoka ili kuendelea na shughuli zao.