Taa zenye kamera zaja kufichua uhalifu barabarani




Taa zenye kamera  zaja kufichua uhalifu barabarani
MRADI wa uwekaji wa taa za barabarani ulio chini ya Kampuni ya tanzu ya Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT Ltd), umetajwa kuwa utapunguza ajali na uhalifu kwenye makutano ya barabara.

Taa hizo zitakazofungwa maeneo mbalimbali nchini, zimewekwa kifaa cha kuhisi uwepo wa gari pamoja na kamera, lengo ni kuwasadia askari wa usalama barabarani kubaini matukio mbalimbali yanayotokea.

Imeelezwa kuwa tayari Zanzibar wamenufaika na mfumo huo, kwani taa  wanazotumia barabarani, zimefungwa kamera huku mikoa mingine ya Tanzania Bara ikihitaji maboresho.

Akizungumza na HabariLeo, Meneja wa Maabara ya Ubunifu DIT, Joyce Mbilinyi, alisema miradi huo wa taa za kuongozea magari umelenga kupunguza foleni, ajali na uhalifu katika makutano ya barabara.


 
''Kwenye taa hizi tumeongeza kifaa kitakachoweza kuhisi uwepo wa gari barabarani, ambacho kitatumika zaidi wakati wa usiku.

“Endapo dereva amefika kwenye makutano ya barabara na taa nyekundu inawaka kumtaka asimame, wakati hakuna magari yoyote yanayopita,  kifaa hiki kitawasha taa ya kijani na  kumuongoza dereva kuendelea na safari yake na kuwasha taa nyekundu upande mwingine,''ameeleza  Mbilinyi.

Pia amesema taa hizo zitapunguza ajali kwa sababu wamelenga kuongeza kamera, ili kuonesha kinachoendelea barabarani, ikiwemo ajali katika eneo husika.


''Kitendo cha kuweka kamera kwenye taa hizi ni kuongeza intelijensia, kupunguza msongamano wa magari na ajali zinazotokea kwenye makutano ya barabara.

“Wakala wa Barabara nchini (TANROAD) ulitueleza kiwa mara nyingi wataalamu wanahitajika kutoka nje kuja kurekebisha mifumo hii,  tunaomba serikali na taasisi nyingine zituamini kwamba tunaweza kuleta mabadiliko,'' amesisitiza Mbilinyi.

Meneja Masoko wa DIT Ltd, Agnes Kimwaga amesema wanatamani teknolojia iwavushe kutoka walipo na kwenda mbali zaidi na kutotegemea trafiki awepo barabarani.

''Taa hizi zitasaidia kupunguza foleni na kusaidia kuongoza magari, lengo  kuwapunguzia kazi polisi wakati wa jua kali na mvua.


 
“Taa hizi zenye kifaa cha kuhisi,  zitaweza kuhisi upande wenye magari mengi na kuyaruhusu kupita,'' amesema Kimwaga

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad