MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imetoa onyo kali kwa kituo cha luninga cha Clouds kwa kurusha maudhui ya kumkejeli Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),Shaka Hamdu Shaka juu ya maagizo aliyoyatoa kwa Jeshi la Polisi nchini.
Pia wamepewa onyo kwa kutangaza maudhui yenye vionjo vya ngono au mapenzi katika kipindi cha ‘Clouds E’, ambayo hayafai kusikilizwa na watoto katika muda ambao watoto wanakuwa sehemu ya wasikilizaji wa vipindi vya televisheni yao.
Akisoma uamuzi huo leo Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Habbi Gunze, alisema kupitia kipindi cha ‘Sentro’ kilichorushwa Juni 6, mwaka huu, kilituhumiwa kufanya mzaha na kuweka riwaya na kibonzo vya kejeli wakati mtangazaji akiwasilisha taarifa ya habari kuhusu agizo alilolitoa Shaka kwa polisi.
“Agizo alilolitoa Shaka kwa jeshi lilikuwa la kumkamata mfanyabiashara wa Mtwara, aliyekuwa anatuhumiwa kuwauzia wakulima wa korosho pembejeo feki. Mtangazaji aliwasilisha taarifa hiyo kwa mzaha, kejeli na upotoshaji kwa jamii hivyo wamekiuka kanuni ya 15(2)(c) za kanuni za mawasiliano ya kielektoniki na posta na maudhui ya utangazaji wa Redio na Televisheni ya mwaka 2018,” alisema Gunze.
Alisema kitendo cha kituo hicho kutangaza maudhui yasiyo na staha na yenye viashiria vya ufanyaji wa ngono na yasiyofaa kwa watoto wamekiuka kanuni za 11(1)(c),11(2)(b),12(1)(a),(b),(d) na 14(a)(c) za kanuni za mawasiliano na ya kielektroniki na Posta ya mwaka 2018.
Alieleza kuwa kamati ya maudhui imefanya tathmini na kubaini kituo hicho kuwa kimetenda kosa hilo kwa uzembe kutangaza maudhui yasiyokuwa na staha, yenye lugha ya matusi, viashiria vya ngono na yasiyofaa kwa watoto.
“Kamati imebaini kuwa kituo hicho kilikosa usimamizi makini na hivyo kuruhusu maudhui hasi na yasiyofaa na staha kutangazwa hewani katika muda ambao watoto wanaweza kuwa sehemu ya watazamaji,” alisisitiza Gunze na kuongeza;
"Kamati imekitaka kituo hiki kuzingatia misingi, sheria, kanuni, maadili,weledi, vigezo na viwango vya tasnia ya uandishi na utangazaji wa habari katika kutayarisha, kusimamia na kutangaza vipindi vya taarifa na maudhui mengine kwa ujumla."
Alivitaka vyombo vyote vya habari nchini kuhakikisha wanazingatia utaratibu na ubora unaokubalika wa uwasilishaji wa taarifa za habari kwa kuzingatia maandalizi na usimamizi makini wa vipindi vyao na kutumia lugha fasaha yenye staha katika uwasilishaji wa maudhui.