Ikiwa zimepita wiki mbili tangu msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Raymond Mwayakyusa'Rayvanny', kuachana na lebo ya WCB, ameonekana viunga vya ofisi za Basata pamoja na aliyekuwa bosi wake Naseeb Abdul 'Diamond'.
Dar es Salaam. Ikiwa zimepita wiki mbili tangu msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Raymond Mwayakyusa'Rayvanny', kuachana na lebo ya WCB, ameonekana viunga vya ofisi za Basata pamoja na aliyekuwa bosi wake Naseeb Abdul 'Diamond'.
Julai 12, 2022 Rayvanny kupitia ukurasa wake wa Instagram alitangaza kuachana na lebo hiyo na badala yake atakuwa kwenye lebo yake ya Next level Music (NLM) aliyoianzisha Machi 2021 huku akieleza ni mafanikio ya kukua kwa mtoto.
Pamoja na kuaga huko Mwananchi ilishuhudia leo Jumatano Julai 27,2022 kukiwa na kikao kizito kilichokuwa kikiendelea ofisi za baraza hilo kikimuhusisha msanii huyo na bosi wake Diamond Platnumz'.
Mwananchi iliyofika kwenye ofisi hizo saa saba mchana iliwakuta walinzi wa Diamond Platnumz, wakiwa chumba cha mapokezi wamekaa kwenye viti na walikuwa wameva suti nyeusi mashati meupe ndani na miwani.
Hata hivyo, ilipofika saa kumi ilimuona msanii Rayvanny aliyekuwa amevaa sweta jeusi akiwa anapita katika kordo za ofisi za baraza hilo akiingia na kutoka kwenye vyumba tofauti vya ofisi hizo akiwa ameongozana na baadhi ya watu wasiopungua wanne.
Baada ya muda mfupi, Katibu Mtendaji wa Basata, Dk Kedmon Mapana na baadhi ya maofisa wa Basata alionekana wakiwa na vikao vya nje hali iliyoonyesha kuwa kulikuwa na jambo zito linaloendelea katika kikao hicho.
Hata hivyo, Diamond katika kipindi chote hicho alikuwa ndani ya ofisi ya Katibu wa Basata na ilipofika saa 11 jioni meneja wake Salam CK alitoka nje na kusimama kwa dakika kadhaa barazani.
Kisha alielekea chumba alichokuwepo Rayvanny na haikupita muda Katibu wa Basata alitoka naye ambapo aliwafuata waandishi wa habari wa Mwananchi kuwalalamikia kuwa nani kawaruhusu kuja kurekodi tukio hilo na kamera kwa kuwa kilikuwa ni kikao cha ndani na wasingependa kiripotiwe kokote.
Alimtaka mpiga picha kuacha kufanya kazi yake kwa kuwa ni kikao cha ndani.
Saa 12:56 jioni ilipofika, wote kwa pamoja kwa nyakati tofauti waliondoka na hakukuwa na taarifa za kipi kiliwapeleka Basata.