TUCTA: Kumwongezea mtu Sh. 8,000 ni dhihaka kwa mfanyakazi




RAIS wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, amesema kitendo cha kumwongezea mtu Sh. 8,000 licha ya kutoongezewa mshahara kwa miaka saba, “ni dhihaka kwa wafanyakazi.” Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea)

Rais huyo ameyasema hayo leo Jumanne tarehe 26 Julai, 2022, mara baada ya kumalizika kwa kikao chao na viongozi wa Serikali kujadiliana kuhusu nyongeza ya mishahara ambayo imeleta sintofahamu baada ya kuonekana kuwa ni kidogo tofauti na matarajio ya watumishi.

Amesema kwa leo wamefikia hatua ya kuwaonesha ni kitu gani ambacho hawakukitarajia katika nyigoza ya mishahara.

“Hiyo nyongeza aliyoitaja Mheshimiwa Rais ya asilimia 23.3 kwa namna moja au nyingine tulitarajia itawagusa watumishi wenye vima vyote vya msharaha kwa viwango vilivyozoeleka, lakini kwa bahati mbaya viwango vimekuwa vya chini ambavyo vimewaumiza sana watumishi wa umma,” amesema Nyamhokya.


 
Amesema watu “walifurahi sana walivyotajiwa kile kiwango lakini naamini kwenye utekelezaji haikwenda kama ambavyo dhamira ya Mheshimiwa Rais ilikuwa imedhamiria.”

Nyamuhokya amesema asilimia kubwa wenye kima cha juu cha mshahara wameongezewa Sh 12,000 baada ya kodi huku wengine wakidai kuongezewa hadi Sh 8,000.

“Wengine wamesema wamekutana na Sh 8,000 kiasi ambacho kimeshangaza kwa kweli kwa mtu ambaye hajaongezewa mshahara miaka sita, saba kuongezewa Sh. 8,000 ni dhihaka kwa mfanyakazi,” amesema.


Ameongeza kuwa katika kikao hicho wameiomba Serikali wakakae tena na kutizama ni kitu gani ambacho kinatakiwa kifanyike kama ambavyo imekuwa ikifanyika miaka ya nyuma.

“Tumekuwa tukiongeza mishahara miaka ya nyuma kwasababu nyongeza ya mishahara haijaanza leo imenza zamani isipokuwa hivi karibuni ilisimama na ni muda mrefu wafanyakazi hawajapata nyongeza,” amesema Nyamuhokya.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano huo uliofanyika jijini Dodoma, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema hatozungumzia kilichojiri katika mazungumzo hayo hadi pale watakapofika mwisho wa mazungumzo.

Amesema viongozi wa TUCTA wameomba wakajadiliane wenyewe na kisha watarudi kuendelea na mazungumzo hayo.


 
Katika Sherehe za Mei Mosi mwaka huu zilizofanyika Kitaifa jijini Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan aliwaahidi wafanyakazi kuwa atapandisha mshahara baada ya kupiga hesabu na kujua uwezo wa Serikali.

Baadae katika bajeti wa Fedha na Mipango Waziri Mwigulu Nchemba alitaja ongezeko la asilimia 23.3 ya kima cha chini cha mshahara jambo ambalo liliibua shangwe kwa watumishi wa umma.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad