Mwanaume huyu aonekana akinunua bidhaa kwenye duka kubwa la mjini New York, Julai 27, 2022. Picha ya AP
Mwanaume huyu aonekana akinunua bidhaa kwenye duka kubwa la mjini New York, Julai 27, 2022. Picha ya AP
Uchumi wa Marekani ulipungua kwa robo ya pili mfululizo kati ya mwezi Aprili na Juni, kulingana na takwimu rasmi zilitolewa Alhamisi, na kuongeza hofu ya kudorora kwa uchumi na kusababisha matatizo zaidi kwa Rais Joe Biden kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula.
Pato la taifa kwa kiwango cha kila mwaka lilishuka chini ya sufuri kwa asilimia 0.9 katika robo ya pili, kufuatia kushuka kwa uchumi kwa kiwango kikubwa katika miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu, kulingana na wizara ya biashara ya Marekani.
Ingawa sio ufafanuzi rasmi, ukuaji wa uchumi ukiwa chini ya sufuri kwa robo mbili, kwa kawaida inaonekana kama ishara tosha kwamba mdororo wa uchumi unakaribia, na kudidimia kwa uchumi katika taifa lenye uchumi mkubwa zaidi duniani, kutakuwa na athari za kimataifa, kadhalika athari za kisiasa ndani ya nchi.
Rais Biden amesisitiza kwamba uchumi wa Marekani uko kwenye “nafasi nzuri” licha ya kudorora, akisifu soko imara la ajira.
“Hii haionekani kama mdororo wa kiuchumi kwangu,” amesema katika hotuba yake katika White House, akisisitiza kwamba kiwango cha ukosefu wa ajira kinakaribia rekodi ya kuwa chini sana na zaidi ya ajira milioni 1 ziliundwa katika robo ya hivi karibuni.
Baada ya kupungua kwa asilimia 1.6 katika kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya mwaka, ripoti ya wizara ya biashara imesema kupungua huko kwa kasi katika robo ya hivi karibuni kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na kushuka kwa matumzi ya serikali kwenye ngazi zote, katika uwekezaji binafsi wa bidhaa ikiwemo magari, na kwenye majengo ya makazi, licha ya kuongezeka kwa mauzo ya nje.