Masasi. “Hivi ndivyo inavyotokea, hata ukilima ukajikata kidole huachi kulima maana kula ni lazima, maisha lazima yaendelee,” anasema Halima Mbwana, dereva wa mabasi ya Super Feo aliyepata ajali na kukatika mkono.
Ikiwa ni zaidi ya siku 40 tangu Halima (33), mkazi wa Masasi na dereva wa mabasi ya kampuni ya Super Feo apate ajali iliyomsababishia ulemavu baada ya kukatika mkono wake wa kulia, anasema kuwa hajakata tamaa.
Anasema licha ya ajali hiyo kufifiza ndoto zake za kuwa dereva bora zilizokuwa zimeanza kuchomoza na kumpa umaarufu mkubwa, bado hajakata tamaa.
Akiwa katika mahojiano maalumu na gazeti hili hivi karibuni wilayani Masasi mkoani Mtwara, Halima anasema bado hajakata tamaa na anatamani kurejea kwenye kazi yake hata kwa kupata mkono wa bandia.
“Asilimia kubwa ya Watanzania wanaamini kwamba ile ajali ilifanywa na watu kwa ajili yangu, binafsi ninaamini Mungu alipanga yanikute na sina wasiwasi, nipo hai kama unavyoniona.
“Nafikiri upo mkono bandia unaohisi (censor), kuna dereva mwenzangu naye alikatika mkono, akaniambia hiyo mikono inapatikana Dodoma naweza nikafanya kazi.
Halima, mama wa watoto watatu, anasema alianza kazi mwaka jana katika kampuni ya Super Feo yenye magari yanayofanya safari kati ya Ruvuma, Mtwana na Dar es Salaam.
Ajali ilivyotokea
Halima anasimulia jinsi tukio lilivyotokea, akisema gari alilopangiwa halikuwa lake, kwani dereva husika hakuwepo.
“Unajua wakati napata ajali gari nililokuwa naendesha halikuwa langu, dereva wa gari hilo ambalo lilikuwa linapita Iringa kuja Songea alikuwa na dharura, hivyo nikaambiwa nilichukue hilo gari.
“Nilikwenda salama mpaka Dar kisha nikarudi salama Tunduru na nikageuka ili nikamkabidhi gari lake, lakini kwa mapenzi ya Mungu sikufanikiwa kulikamilisha hilo,” anasema.
Anasema ajali hiyo ilitokea katika Kijiji cha Huria, Wilaya ya Tunduru ambapo eneo hilo lina kona nyingi zenye muundo wa ‘S’.
“Nilishangaa kumuona mtu ninaemfahamu kabisa, ni dereva mwenzangu mbele yangu anakatisha barabara. Nikajiuliza anafanya nini maeneo yale?
“Nilitahaharuki kwa nini awepo maeneo yale ikabidi nimkwepe nisimgonge nikawa nakwepea kulia huku gari linanivuta kushoto, ambapo kuna mkorosho na ujenzi wa mitaro unaendelea nikahofia kuharibu gari na kuumiza abiria. Nikafanikiwa kuiangusha kwenye majani ili kuepusha uharibifu na watu kuumia,” anasema.
Anaendelea; “Kwa kweli nilipambana hadi nilisimamia usukani kabisa ili kuepusha ajali, kiudereva tunaita kuipiga mtama, nilifanikiwa kwa kuwa ilikuwa kwenye majani na uharibifu haukuwa mkubwa sana, japo iliteleza kidogo na kuusaga mkono wangu.
“Nilipokuwa nasoma niliambiwa kwamba, ukifika eneo ukipata kitu chochote, lazima uzime gari. Hivyo, pamoja na kuuona mkono wangu wa kulia ukiwa umesagika, nilitumia mkono wangu wa kushoto kuzima gari ili kuepusha madhara mengine,” anasema.
Hata hivyo, anasema alisaidiwa na kijana aliyekuwa mhudumu wa basi hilo kwa kumnyanyua alipokuwepo na kumtoa nje, huku pia akisaidiana na abiria wengine kutoka nje na baadaye walipelekwa hospitali iliyokuwa karibu.
“Mkono wangu hakumwaga damu sana, mishipa ilisagika haikukatika hivyo sikupoteza fahamu.
“Baada ya kuokolewa nilikaa kuwaangalia abiria wangu wakiokolewa, bahati nzuri wote walikuwa salama hawakuumia sana na hakuna aliyefariki, nadhani ningeumia sana kama ningepoteza mtu,” anasimulia.
“Halikuwa tukio zuri, lakini kwa sababu hakuna aliyepoteza maisha ilinifariji mno.”
Visa na mikasa barabarani
Akisimulia zaidi kuhusu mikasa inayowakumba madereva barabarani, Halima anasema hukutana na mauzauza mengi yanayowafanya washikwe na butwaa.
“Siku moja nikiwa wilayani Tunduru katika eneo la mto Muhesi niliona bibi yangu mzaa mama akipita mbele ya gari wakati nikiwa kwenye mwendo kasi, niilishangaa nikaishia kusema bibi, lakini nikakumbuka kuwa hayupo Tanzania yupo Oman nikaendelea na safari nikajua ni mauzauza safarini,” anasema.
Anakumbuka pia kisa kingine ambapo akiwa kwenye mwendo wa haraka, alimwona dereva mwenzake ambaye anasema ni mtu wake wa karibu akikatisha barabarani
“Nikahisi ameharibikiwa gari au anatafuta maji au mawe ili asaidie gari. Yaani nilichanganyiwa na niliyumba sana nikapambana gari likasimama.
“Tukio hilo lilinifanya niwe chizi, maombi ndio yaliyonisaidia kwa kiasi kikubwa, nilipimwa magonjwa yote lakini hawakuona shida.
Kuhusu kampuni anayofanyia kazi, anamshukuru mmiliki wake akisema bado hajamwacha, japo gari yake iliumia na bado lilikuwa jipya. “Kila baada ya siku tatu malipo ya matibabu yalikuwa yanakuja,” anasema.
“Baadhi ya madereva walinitenga kwa kuwa mimi ni mtoto wa kike, wengi wao hawakuwa na ushirikiano na mimi, nimepitia magumu mengi, niliwahi kuzimia barabarani kwa manyanyaso ya baadhi ya mamlaka za barabarani.
Safari ya udereva
Anasema alianza kazi kwenye magari mwaka 2009 kama kondakta katika kampuni ya Country yaliyokuwa yakifanya safari zake kati ya Dar-Newala.
Baadaye aliajiriwa na kampuni ya Hamanju mwaka 2010, Maning Nice 2013, baadaye akaajiriwa Machinga.
Nikaona kuna umuhimu wa kupanda hatua nyingine, nikaenda kupata mafunzo ya udereva katika Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na baadaye kupata mafunzo maalumu yaitwayo Sub Scania kwa ajili ya madereva wa magari makubwa. “Mwaka 2019 safari yangu ya udereva ilianza katika Kampuni ya Mining Nice kati ya Dar-Mtwara, Dar - Masasi na baadaye Tunduru, urefu wa kilomita 850.
Mama mzazi wa Halima
Kwa upande wake Nura Mohamed Abdallah (mama mzazi wa Halima) anasema ajali hiyo imemfunza vitu vingi, ikiwamo imani.
“Nilipoipokea taarifa ya ajali yake nilitaharuki, ndio nilikuwa nataka kunywa chai saa tatu asubuhi nililia sana, lakini baadaye niliacha kulia kwa kuwa niliamini nitamvunja moyo mwanangu .
“Nilifika hospitali na kumkuta ndiyo ametoka chumba cha upasuaji, aliponiona alitaka kulia lakini nilimpa moyo ili ayakabidhi maisha yake kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwa ndiye anapanga uishi vipi na uweje maishani mwako.
“Mgonjwa wetu kwa sasa amepona na anaendelea vizuri kwa sasa hadi amesafiri kwenda kazini kwake ambapo walikuwa wanamhudumia kwa ukaribu zaidi, kwa kweli wametufaa,” anasema Nura.
Kuhusu alivyolipokea wazo la mwanaye kuwa dereva wa magari makubwa anasema: “Wakati anaanza kazi ya udereva sikumshangaa kwa kuwa ndiyo kazi aliyokuwa akifanya baba yake, niliipokea kawaida na sikuwa na hofu juu yake kwa kuwa ni mtoto ambaye anajituma katika kazi na alienda akasomea udereva na akamaliza salama na kuanza kuendesha magari makubwa,” anasema Nura.