Wabunge waijia juu Toyota Tanzania, Spika aomba majibu




Gari aina ya Toyota Land cruiser V8
SPIKA wa Bunge la Tanzania, Dk. Tulia Akson, ameitaka Serikali kutoa majibu hoja ya suala la Serikali kushindwa kuagiza magari moja kwa moja kutoka kwa mzalishaji na badala yake kutumia wakala. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Dk. Tulia amesema hoja hiyo inafanana na suala la uagizaji wa mafuta ambayo mara nyingi hutumia mawakala badala ya kwenda kwa wazalishaji moja kwa moja.

Spika ameyasema hayo leo Alhamisi tarehe 23 Juni, 2022 baada ya Mbunge wa Viti Maalum, Riziki Lulida kuhoji sababu ya Toyota Tanzania kumiliki soko na kusababisha watanzania kushindwa kununua magari mapya kiwandani.

“Kama ndivyo Waziri atakuja kutuambia, najua huwezi kujibu hoja zote lakini hili tungependa kuisikia kwamba watu hawawezi kuagiza magari zero mileage bila kupitia Toyota litakuwa jambo la ajabu sana,” amesema.


 

Spika amesema jambo hili linafanana na lile la mafuta kwamba huwezi kwenda moja kwa moja kwa wazalishaji, “sasa kama inawezekana ni vizuri watanzania wajue ili wachangamkie fursa hiyo.”

Awali akichangia hoja hiyo Lulida amesema wakala wanauza magari wameingia makubaliano na wazalishaji nchini Japan ya kuzuia mtu kununua gari jipya moja kwa moja hadi apitie kwao.

Ameongeza kuwa gharama ya kununua gari Tanzania ni mara mbili ya bei wanayonunua Kenya na Uganda.


“Tumefika wapi tujitambue, kwanini tunaendelea kuchezewa namna hii,” amesema na kuongeza kuwa yeye ni mwathirika wa kununua magari mapya ya Toyota kwa bei mara mbili ya ile inayouzwa Kenya.
“Nataka Waziri ajibu hoja hii.”


Amesema UNDP ni taasisi inayoleta magari taznaia kwaajili ya miradi yao lakini hata wao wamezuiwa kununua gari jipya kutoka kwa wazalishaji na kutaka Sheria ya Manunuzi ya mwaka 2013 kubadilishwa kwani “ni mwiiba kwa nchini hii”.

“Haikubaliki tunaangaika kutafuta fedha kutoka kwa wananchi masikini halafu mwisho mtu mmoja anachukua donge lote anakaa nalo pembeni, tusikubali muda wa kutufanya shamba la bibi limepitwa na wakati watanzania sasa tumefunguka tunataka maonevu yote yanashughulikiwa,” amesema.

Mbali na Lulida Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku, ametoa mfano wa yeye mwenyewe kununua gari mara mbili ya bei za kawaida.

“Leo ukitaka kuagiza Toyota mpya kama hili la Waziri wa Fedha inauzwa dola 140,000 pamoja na ushuru lakini mimi nikiiagiza hiyo gari ushuru wake tu ni Sh210 milioni halafu kununua dola 140,000, yaani ushuru umewekwa mara mbili ili ulazimike kupitia Toyota,” amesema.

Naye mbunge wa Manyoni Magharibu, Yahaya Massare, amesema Toyota Tanzania ni wakala wa mzalishaji aliyepo Japan hivyo amemiliki soko “kiasi kwamba wewe huweza kwenda kule kwenye soko.”

Amesema hoja ya Lulida ni kwamba “kuna uvivu tu wa watu wetu wamekubali kuingia kwenye mtego wa Toyota Tanzania ambaye ni agent wa mtengenezaji kwanini serikali isiagize kiwandani moja kwa moja?”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad