Mwanga. Wakati mwili wa Ngatipa Parmao (17) anayedaiwa kuuawa na askari ndani ya hifadhi kwa kupigwa risasi ukizikwa, baba mzazi wa mtoto huyo amemwomba Rais Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mauaji hayo akisema mwanaye aliuawa kwa makusudi.
Pia wazazi hao wamedai kuna mchezo mchafu wa kuharibu ushahidi baada ya vipimo vya awali kabla ya upasuaji kuonyesha kulikuwa na risasi ndani ya mwili lakini baadaye ikaelezwa haijakutwa.
Ngatipa anadaiwa kupigwa risasi Julai 6 mwaka huu na askari wa wa Hifadhi ya Mkomazi, Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro wakati anachunga ng’ombe pembezoni mwa hifadhi hiyo.
Mara baada ya kupigwa risasi, Ngatipa alipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Same kwa matibabu ya awali kisha akahamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) ambako alifariki dunia Julai 8.
Juzi, mwili wa mtoto huyo ulifanyiwa uchunguzi wa sababu ya kifo (postmoterm) na kubainika kuwa na matundu mawili yanayodaiwa kuwa ya risasi katika sehemu ya mkono upande wa kulia na sehemu ya tumboni.
Mazishi ya mtoto huyo yalifanyika jana katika Kijiji cha Pangaroo wilayani Mwanga na kuhudhuriwa na viongozi wa CCM na Serikali akiwemo mkuu wa wilaya hiyo, Abdallah Mwaipaya.
Vilio na simanzi vilitawala wakati jeneza lenye mwili wa mtoto huyo jamii ya Kimaasai ulipowasili kijijini hapo kwa maziko yaliyohudhuriwa na watu mbalimbali.
Kabla ya maziko ya mwanaye, Marius Parmao alisema baada ya kijana wake kupigwa risasi alipekwa hospitali ya same ambako ilibainika kulikuwa na risasi ndani ya mwili.
“Tulikuwa na OCD (mkuu wa molisi wa wilaya) na aliagiza daktari amfanyie mgonjwa vipimo vya uchunguzi, daktari alifanya hivyo na kutuhakikishia kuna risasi. Akatwambia ili upasuaji ufanyike tunapaswa kulipa Sh140,000 na tukafanya hivyo ili mtoto wangu aokolewe maisha,” alisema Parmao kwa lugha ya Kimaasai ikitafsiriwa na Lameck Kipuyo kwa Kiswahili.
Mzee huyo akizungumza taratibu alisema, “baada ya kuhakikisha gharama zote zimelipwa OCD aliondoka na mtuhumiwa kwenda naye kituoni Mwanga, lakini cha kushangaza baada ya upasuaji kufanyika tukaambiwa risasi haionekani, nilipoambiwa hivyo niliumia sana.”
“Kutokana na hali ya mtoto kuendelea kuwa mbaya tuliomba tumpeleke KCMC kwa matibabu zaidi lakini kesho yake mtoto wetu alipoteza maisha,” alisema Mzee huyo mwenye wake watatu na watoto 18.
Alisema kilichofanywa na uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Same si sawa maana hizi ni mbinu za kutuzungusha ili mtoto wetu asipate haki, kutokana na hii naiomba Serikali isimamie haki maana vipimo vilifanyika na tukahakikishiwa risasi ipo ndani.”
Alipotafutwa Mganga mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro (RMO) Jairy Khanga kuhusu tuhuma za hospitali ya wilaya ya Same, alisema amepokea taarifa hiyo na anafuatilia kuchunguza ukweli wake.
Parmao alisema hospitali ya KCMC walipomfanyia postmoterm walibaini kuna matundu mawili ambayo moja lilikuwa upande wa kulia na lingine sehemu ya tumboni.
Hata hivyo alisema, kinachoumiza zaidi mwanaye hakukutwa na ng’ombe hifadhini, walikuwa nje ya hifadhi kwani kutoka eneo walilopokuwa mpaka hifadhini ni kilomita mbili.
“Baada ya ng’ombe 54 aliokuwa nazo mwanangu kukamatwa nilitakiwa nilipe Sh1.3 milioni na nilifanya hivyo wakati mtoto wangu akiwa hospitali, ndipo nikarejeshewa mifugo yangu,” alisema.
DC Mwaipaya aliiomba familia kuwa watulivu wakati Jeshi la Polisi linaendelea kuchunguza tukio hilo na kuwa hadi sasa linawashikilia askari watatu.
“Niwape pole familia kwa hili lililotokea na sisi Serikali tumekuwa nanyi tangu tukio hili limetokea, nashukuru kwa uvumilivu wenu ambao umeonyesha na sisi tuko pamoja nanyi,” alisema.