Waziri Mchegerwa Ang'aka Timu ya Yanga Kutawala tuzo



WAKATI Yanga ikiendeleza ubabe kwa kutwaa tuzo mbalimbali zilizotolewa kwa waliofanya vizuri katika msimu wa 2021/2022, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amelitaka Baraza la Michezo Taifa (BMT),...

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa.
... kuchukua hatua kali kwa kiongozi yoyote atakayebainika kuvunja maadili ndani ya sekta hiyo.

Mchengerwa alisema hayo kwenye hafla ya utoaji tuzo za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambayo ilifanyika jijini Dar es Salaam juzi usiku.

Waziri huyo alisema amewataka viongozi wa klabu zote hapa nchini kuzingatia maadili na kuachana na vitendo vya utovu wa nidhamu ambavyo havisaidii kupiga hatua katika maendeleo ya michezo hapa nchini.

“Viongozi wa klabu wanatakiwa kuwa na maadili kwa wenzao, kuna watu wa mpira hawaheshimu viongozi, hili ni jambo la kukemea, nasisitiza BMT kuhakikisha wanawachukulia hatua kali viongozi ambao hawataheshimu wenzao,” alisema na aliongeza;


“Viongozi tunatakiwa kuonyesha maadili ili wachezaji wetu huku nyuma wawe na maadili ya kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa, klabu haziwezi kupiga hatua katika michezo endapo hazitazingatia suala hilo,”.

“Wenzetu wanafanikiwa sana kwenye michezo kwa kuwa wanazingatia maadili na kuheshimiana wenyewe kwa wenyewe, niwahakikishie wizara ninayoongoza sitakubali kuona mtu wa michezo anakosa maadili na kutoheshimu kiongozi, sitalifumbia macho," alisema Mchengerwa.

Alivitaka vilabu vya michezo kufanya uwekezaji ikiwa ni pamoja na kujenga miundombinu ili kuinua michezo.


“Wakati umefika wa klabu na timu za Tanzania kumiliki viwanja vyao kama ilivyo kwa mataifa mengine huko duniani, naomba BMT na TFF, wiki ijayo ratibuni kikao na viongozi wa vilabu tulimalize suala hili, " alisema waziri huyo.

Aliongeza serikali inatarajia kujenga viwanja vya michezo ya ndani na ukumbi wa sanaa katika eneo la Kawe jijini huku akisisitiza sherehe kama hizo za utoaji tuzo mwakani zitafanyika kwenye ukumbi huo wa kisasa.

Aliongeza dhamira ya serikali kwa sasa ni kuifanya michezo kuwa uchumi na tayari imeshatenga fedha kwa ajili ya kukarabati viwanja sita ikiwa ni mikakati ya Tanzania kuandaa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), zitakazofanyika mwaka 2027.

“Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa ya kuendeleza michezo nchini, serikali imedhamiria kufanya maboresho ya viwanja hivyo kwa ajili ya ya kuomba uenyeji wa AFCON kwa mwaka 2027,” Mchengerwa alisema.


Alitaja viwanja sita vitakavyokarabatiwa kwa kuwekewa nyasi za asili ni CCM Kirumba kilichopo jijini Mwanza, Sheikh Amri Abeid (Arusha), CCM Sokoine (Mbeya), CCM Mkwakwani (Tanga), Jamhuri (Dodoma) na Amaan uliopo Zanzibar.

Alisema maboresho hayo ni ya kimkakati na lengo kubwa ni kuona sekta ya michezo inasonga mbele na kuzikumbusha timu kutimiza lengo la kuwa na viwanja vyake.

“Lakini pia wawekezaji na wafanyabiashara huu ndio muda wa kujitokeza kuwekeza katika kuendeleza sekta ya michezo kwa sababu hapo baadae mambo yatakuwa mazuri lakini hamtaweza kupata nafasi ya kuingia kirahisi,” alisema waziri huyo.

Bosi huyo wa michezo aliitaka BMT na TFF kuratibu kikao baina yake na watendaji wakuu wa timu zote za Ligi Kuu Tanzania Bara mapema wiki ijayo ili kujadili namna ya utekelezaji wa suala hilo la miundombinu.


Wadhamini wakuu wa Ligi Kuu NBC iliwakabidhi mabingwa wapya wa ligi hiyo, Yanga hundi ya mfano ya Sh. milioni 100 wakati Simba Queens iliyotwaa taji hilo kwa upande wa wanawake ilikabidhiwa kitita cha Sh. milioni 15 kutoka kwa wadhamini wakuu wa ligi yao, Kampuni ya Bia ya Serengeti.

Tuzo ya Mfungaji Bora ilichukuliwa na straika wa Geita Gold FC, George Mpole, aliyetupia mabao 17 wavuni wakati klabu yake ikimaliza msimu katika nafasi ya nne na tuzo ya Mchezaji Bora wa soka la ufukweni ilikwenda kwa Adel Mohamed, Mchezaji Bora wa First League ni Mohamed Hussein na bao bora la msimu wa 2021/22 lilifungwa na Fiston Mayele wa Yanga wakati wakicheza dhidi ya Biashara United.

Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kombe la FA ilikwenda kwa Abdul Suleiman 'Sopu’ wa Coastal Union huku tuzo ya Mchezaji Bora Ligi ya Wanawake ni Fatuma Maono, ‘Fetty Densa’ wa Simba Queens na Yannick Bangala wa Yanga alishinda kwa upande wa Ligi Kuu, Meneja Bora wa uwanja ni Sikitu Kilakala wa Azam Complex, Chamazi na Kamishna Bora wa Ligi Kuu ni Abousufian Silia huku ile ya beki bora ikienda kwa Hennock Inonga wa Simba.

Seti ya Waamuzi Bora ni ya mchezo wa Mtibwa Sugar dhidi ya Yanga, ambapo ilichezeshwa na Martina Saanya, Mohamed Mkono, Rashid Gongo na Joachim Akamba na tuzo za heshima za Rais wa TFF, Wallace Karia zilienda kwa Bakari Shime, Stephania Kabumba, Salim Amir na Omar Muhaji (marehemu).

Mwamuzi Bora Msaidizi kwa wanawake ni Glory Tesha kwa Ligi Kuu Bara ni Frank Komba huku wa kati ikienda kwa Ahmed Arajiga, Kocha Bora Ligi Kuu ya Wanawake ni Sebastian Nkoma wa Simba Queens na Nesreddine Nabi wa Yanga alikuwa kwa upande wa Ligi Kuu wakati mchezaji chipukizi kwa wanawake ni Clara Luvanga wa Yanga Princess na kwa Ligi Kuu ni Dickson Mhilu wa Kagera Sugar.


Kipa Bora wa Kombe la FA ni Mohammed Mohammed wa Coastal Union na kwa Ligi ya wanawake ni Gelwa Yona wa Simba Queens wakati kikosi bora cha msimu kinaundwa na Djigui Diarra, Djuma Shaaban, Bakari Mwamnyeto, Yannick Bangala, Feisal Salum na Fiston Mayele, (Yanga), Mohamed Hussein, Inonga na Pape Sakho( Simba), Abdul Suleiman ‘Sopu’ (Coastal Union) na George Mpole (Geita Gold FC).

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad