Dar es Salaam. Licha ya klabu za Simba na Azam FC kutimkia nchini Misri kwa ajili ya kuweka kambi za maandalizi ya msimu ujao, upande wa Yanga mambo ni tofauti.
Yanga inadaiwa kuwa tayari kulipa fidia ya Sh200 milioni kwa hoteli na mambo mengine, baada ya kuweka uhakika wa kwenda (booking) na kisha kubatilisha uamuzi huo.
Simba na Azam FC tayari zimeshafika Misri kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao, huku zote zikitarajiwa kurejea nchini mwezi ujao.
Awali, Yanga ilikuwa na mipango ya kuweka kambi nchini Uturuki, kuanzia Julai 15, lakini sasa kumekuwa na mabadiliko ambayo yanaifanya miamba hiyo kubaki nchini.
Habari ambazo Mwananchi limepenyezewa, kocha mkuu wa timu hiyo, Nasreddine Nabi aliwaambia viongozi wa Yanga waachane na suala la kwenda Uturuki ili yasitokee kama yale ya msimu uliopita walipokwenda Morocco na badala yake wabaki nchini ili wapate muda wa kufanya maandalizi ya kutosha.
Nabi hataki shida iliyotokea msimu uliopita, ambayo anaamini iliathiri kikosi chake katika mashindano ya kimataifa kwa kutokuwa na wachezaji wote.
Yanga ilijikuta ikikosa wachezaji wote na kuanza nusu maandalizi, kitu ambacho kocha Nabi anaamini kilichangia pia kufungwa na Rivers United ya Nigeria kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Inaelezwa kuwa tayari Yanga ilishaweka mipango ya kwenda Uturuki na kuweka oda kabisa ya sehemu ya kufikia, lakini Uongozi wa timu hiyo upo tayari kulipa fidia baada ya kubadilisha uamuzi.
Wachezaji wa Yanga wanatarajia kuanza kuingia kambini kuanzia tarehe 22 mwezi huu kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya.
Mmoja wa mabosi wa Yanga alilidokeza gazeti hili kuwa timu hiyo haitaondoka nchini, huku wakiwa kwenye vikao kuamua kuendelea na kambi ya Avic Town, Kigamboni, au kwenda Black Rhindo, Karatu.
“Hadi sasa, asilimia kubwa ya timu kukaa kambini hapa hapa nyumbani, tunaangalia kama ni Avic au Karatu na hili linafanyika ili wachezaji wote wakutane kwa pamoja kwa sababu wengine wanatoka kwenye nchi ambazo inachukua muda mrefu kuingia Uturuki,” alisema bosi huyo.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli ili azungumzie suala la wao kuweka kambi alisema; “Kambi bado, tutatoa taarifa rasmi.”
Yanga imekamilisha usajili wake wa msimu huu, baada ya jana alfajiri kumtambulisha nyota wake wa mwisho, Stephane Aziz Ki, aliyesajiliwa kutoka Asec Mimosas.
Ki anaungana na Lazarous Kambole, Bernard Morrison, Gael Bigirina na Joyce Lomalisa katika usajili wa nyota wapya waliojiunga na klabu hiyo msimu huu.