Kuelekea mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao, uongozi wa mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, Yanga umechimba mkwara mzito kwa kusema tayari umeanza kufanya maandalizi mazito ya ndani na nje ya uwanja kuhakikisha wanaandika rekodi ya kufika mbali katika michuano hiyo.
Yanga tayari imekata tiketi ya uwakilishi wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufanikiwa kutawazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu msimu huu, huku wakiandika rekodi ya kushinda ubingwa huo mara 28.
Katika michuano hiyo msimu uliopita Yanga waliondolewa katika hatua ya awali, mara baada ya kukubali kipigo cha jumla cha mabao 2-0 kutoka kwa Rivers United ya Nigeria, ambapo walifungwa bao moja nyumbani na moja ugenini.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Yanga, Injinia Hersi Said amesema tunafahamu kuwa mashindano ya kimataifa sio jambo dogo, ni wazi kuwa tunapaswa kufanya kazi kubwa ili kupata mafanikio katika mashindano hayo kwa kuwa tunakutana na timu bora zaidi kutoka mataifa mengine.
“Lakini nataka niwaambie kuwa sisi hatufanyi masikhara tumejipanga kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea, tunajua wazi kuwa msimu uliopita tuliondolewa katika hatua ya awali na hatutaki kuona hilo likitokea msimu huu.