Achana na Matokeo Kufungwa na Vipers, Yanga Yafunika Wiki ya Mwananchi



Wachezaji wa Yanga wakiingia uwanja wa Benjamin Makapa jana kwenye kilele cha wiki ya Mwananchi
ACHANA na matokeo ya Yanga kufungwa 0-2 na wageni wao Vipers FC, ukweli ni kwamba, Wananchi jana walifunika katika suala zima la kuhitimisha kilele cha Tamasha la Wiki ya Mwananchi.

Kabla ya Yanga kupoteza mchezo huo wa kirafiki dhidi ya Vipers, zilifanyika burudani kadhaa ikiwemo utambulisho wa mastaa wa kikosi hicho.

Miongoni mwa wachezaji walioteka shoo wakati wa utambulisho, ni wachezaji wapya akiwemo Stephane Aziz Ki na Bernard Morrison.

Aziz Ki ambaye amejiunga na Yanga akitokea ASEC Mimosas, alikuwa mtu wa mwisho kutambulishwa na kushangiliwa kwa shangwe kubwa uwanja mzima.


 
Kabla ya Aziz Ki, alitangulia Morrison ambaye alianza kwa kuwaomba radhi mashabiki wa Yanga akisema: “Nisameheeni, najua niliwaudhi wakati naondoka. “Niliwahi kusema kwamba nimeenda Simba ambapo ni chuo kikuu cha soka Tanzania, sasa niwaambie kwamba nimerudi Yanga kuja kusomea masters, hiki ndiyo chuo kikubwa zaidi.

“Nimefurahi kuona kocha mkubwa Afrika, Pitso Mosimane yupo hapa, nimwambie tu, amekutana na Kocha Bora wa Tanzania, Nasreddine Nabi.” Baada ya kuzungumza hayo, Morrison aliibua shangwe uwanja mzima ambapo mashabiki walimshangilia na kuonesha kwamba wamemsamehe.


                                          Mchezaji wa Yanga Azizi Ki
Wengine walioibua shangwe wakati wa kutambulishwa ni Yannick Bangala, Feisal Salum, Fiston Mayele na Gael Bigirimana.


SAPRAIZI YA MANARA Wakati wengi wakifahamu kwamba Haji Manara ambaye amefungiwa kujihusisha na soka kwa kipindi cha miaka miwili kutokana na kukutwa na hatia juu ya masuala ya kinidhamu, jana alifanya sapraizi ya kutosha. Wakati Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikitoa adhabu kwa Manara Julai 21, mwaka huu, ilisema hatakiwi kujihusisha na masuala ya soka, hivyo hatakuwepo katika Tamasha la Mwananchi, lakini jana aliibuka.

Manara aliingia uwanjani akisindikizwa na walinzi, kisha akachukua jukumu la kutambulisha kikosi cha Yanga kuanzia benchi la ufundi hadi wachezaji, kisha akaaga akisema anaondoka kwani alialikwa kuwa mshereheshaji tu.

Stori: Marco Mzumbe

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad