Agizo la Polisi kwa Wamiliki wa Shule



Dar es Salaam. Wamiliki wa magari ya shule wametakiwa kuyapeleka magari yao kwa ajili ya ukaguzi na watakaokaidi hatua kali zitachukuliwa.

Agizo hilo lilitolewa jana na Kamanda wa Polisi, Kitengo cha Usalama Barabarani, Wilbroad Mutafungwa katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akikagua baadhi ya magari ya shule na kusema suala hilo ni la lazima na lipo kwa mujibu wa sheria.

Licha ya kamanda huyo kueleza ukaguzi huo ni wa kawaida kwa mujibu wa sheria, unafanyika wiki moja tangu gari la Shule ya Msingi King David, Mkoa wa Mtwara kupata ajali na kusababisha vifo vya wanafunzi 11 na watu wazima wawili, huku 15 wakijeruhiwa.

Ajali hiyo iliibua mjadala unaotokana na idadi ya wanafunzi waliokuwa wamebebwa katika gari hilo na ukubwa, kwani ni aina ya hiace ambayo ina uwezo wa kubeba watu wasiozidi 15.


Magari mengi ya wanafunzi yamekuwa yakionekana kubeba wanafunzi wengi, huku mengine yakionekana mabovu.

Jana, Kamanda Mutafungwa alisema magari yote ambayo hayajakaguliwa hayataruhusiwa kuingia barabarani kipindi shule zitakapofunguliwa. Alisema sheria ya usalama wa barabarani inasema magari ya shule yanatakiwa kukaguliwa mara mbili kwa mwaka na pale inapobidi.

Mutafungwa alisema katika ukaguzi huo wamejikita kukagua ubora wa bodi ya gari, matairi, mifumo ya usukani, breki, kukagua viti pamoja na mifumo mingine ambayo haifanyi kazi katika gari na kuchukua hatua madhubuti.


Injinia Yona Afrika kutoka Baraza la Taifa la Usalama wa Barabarani alisema kazi yao ni kusimamia usalama wa barabarani, kuweka miongozo na kuangalia sheria zote zinazohusiana na usalama barabarani.

Kwa upande wake, Ofisa leseni Mkoa wa Dar es Salaam, Mansul Ommary alisema katika ukaguzi huo wanakagua vibali vyao pamoja na masharti mbalimbali ya leseni.

“Magari yote ya shule lazima yapakwe rangi ya njano pamoja na kuandikwa maandishi yanayoonekana, ikitambulisha kuwa ni magari ya shule,” alisema Ommary.

Pamoja na hayo, katika Mkoa wa Mara magari 10 yanayosafirisha wanafunzi yameondolewa barabarani baada ya kubainika kuwa na matatizo ya kiufundi.


Uamuzi huo ulitangazwa na mkuu wa kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Mara, Mathew Ntakije baada ya ukaguzi wa magari ya wanafunzi uliofanyika katika Wilaya za Musoma, Serengeti, Bunda na Butiama.

“Tulikagua magari 61, kati ya hayo, magari 10 yalibainika kuwa na ubovu na matatizo ya kiufundi yanayohatarisha usalama na maisha ya watumiaji, tumeng’oa pleti namba za magari hayo kuyazuia kutumika,” alisema Ntakije.

Mkoani Njombe magari 13 yamekaguliwa, huku mkaguzi wa magari hayo ambaye ni kamanda kikosi cha usalama barabarani mkoani humo, Sajenti Raphael Raphael akisema baadhi yamekutwa na dosari, zikiwemo mfumo wa usukani, uchakavu wa magurudumu, uchakavu wa mabodi na mawasiliano upande wa umeme.

“Kuna baadhi ya magari yanavuja kwenye mfumo wa injini, bado tunaendelea na ukaguzi kwenye magari mengine,” alisema Raphael. Wakati hayo yakifanyika, madereva wa mabasi hayo wameiomba Serikali kuboresha barabara, ili kupunguza ajali zinazosababishwa na ubovu wa barabara.


Akizungumzia suala hilo, Dk Amos Mcherwa, mmoja wa wamiliki wa shule alisema, “zoezi hili ni zuri, lakini wakati mwingine hatuhitaji kuambiwa, polisi wanatakiwa wafanye kwa kushtukiza.”

Ukaguzi huo umeanza jana ikiwa ni siku moja tangu kutangazwa na unatarajiwa kudumu kipindi chote cha likizo.

Imeandikwa na Emmanuel Msabaha, Aurea Simtowe, Jackson Ngowo (Dar), Beldina Nyakeka (Iringa) na Seif Jumanne (Njombe).

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad