Ajali ya basi yaua watano, 15 wajeruhiwa




WATU watano wamefariki dunia akiwamo Diwani wa Viti Maalum kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wengine 15 kujeruhiwa baada ya basi la kampuni ya Tanzanite kupinduka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Stella Mutabihirwa, ajali hiyo ilitokea majira ya saa 9:30 alasiri katika kijiji cha Mbwasi, wilayani Manyoni barabara ya Singida-Dodoma na ilihusisha basi la Tanzanite lenye namba za usajili T916 DNU.

Aliwataja waliofariki kuwa ni Mwinjuka Mkumbo (40) ambaye ni Diwani wa Viti Maalum CCM Wilaya ya Iramba, Alicia Flagence, mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na wengine watatu ambao majina yao bado hayajatambulika.

Kamanda huyo alisema, majeruhi wa ajali hiyo walikimbizwa katika Hospitali ya Rufani Dodoma, na kwamba diwani huyo alifariki wakati akipatiwa matibabu, huku wengie 11 wakiruhusiwa.

Aliwataja majeruhi wanaoendelea na matibabu ni Sharifati Mwipi (32), Rudia Kadila (59), Said Mbwana (39) na Abdul Ramadhani (32), huku Mwamba Sita (26) alihamishiwa Hospitali ya Benjamini Mkapa, Dodoma.


Vilevile, alisema uchunguzi wa awali ulibaini kuwa chanzo cha ajali ni mwendokasi wa dereva wa basi hilo, Abdul Kingwande, aliyeshindwa kulimudu kuacha njia na kupinduka.

Kamanda Mutabihirwa, alisema polisi wanamtafuta dereva wa basi hilo ambaye alitoroka muda mfupi baada ya ajali.

"Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linatoa wito kwa madereva wote wa vyombo vya usafiri kuhakikisha wanazingatia sheria za usalama barabarani ili kuepukana na ajali," alisema.


Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Innocent Msengi, alisema wamepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha diwani huyo kwa kuwa alikuwa msaada mkubwa kwa halmashauri kutekeleza majukumu yake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad