JESHI la Polisi nchini kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani limetangaza kuanza oparesheni kukagua magari na kuwachukulia hatua za kisheria madereva wanaofanya makosa barabarani.
Jeshi hilo limetangaza oparesheni hiyo siku chache baada ya mfululizo wa ajali za barabarani katika mikoa ya Mtwara, Tanga, Singida, Shinyanga na Mbeya kuua watu zaidi ya 50. Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani nchini, Wilbroad Mutafungwa alisema hayo jana alipofanya ziara kukagua kituo cha ukaguzi wa malori kinachojengwa Inyala mkoani Mbeya.
Kituo hicho kinajengwa jirani na ilipotokea ajali iliyoua watu 19 Jumanne wiki hii baada ya lori kufeli breki na kugonga magari matatu.
Kamanda Mutafungwa alisema jeshi hilo linaandaa mpango kazi maalumu wa askari kushughulikia makosa hayo ili kumaliza ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya wananchi.
Aliyataja makosa watakayoshughulika nayo ni magari ya mizigo kubeba abiria, magari ya abiria kujaza watu kupita uwezo wao, matrekta na mikokoteni kuingia barabarani bila kuwa na alama za usalama.
“Tutashughulika na makosa yote haya pamoja na kukagua mifumo ya magari ili kuhakikisha ajali hizi tunazimaliza, kwa hiyo niwatangazie kwamba katika kipindi hiki tutakuwa wakali kupita kiasi kwa wale wanaokiuka sheria,” alisema Kamanda Mutafungwa.
Aidha, aliuomba Wakala ya Barabara Tanzania (Tanroads) ukamilishe haraka ujenzi wa kituo cha ukaguzi wa malori cha Inyala. Alisema ajali zinazotokea eneo hilo zimegharimu maisha ya watu na kuharibu vyombo vya usafiri kutokana na mteremko huo.
“Lakini pia tunaomba wenzetu Tanroads watusaidie kuweka alama za usalama barabarani kwenye maeneo haya yenye mteremko na kwenye lile daraja ilipotokea ajali wanatakiwa watuwekee kingo,” alisema Kamanda Mutafungwa. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Ulrich Matei aliwatembelea majeruhi wa ajali hiyo katika hospitali mbalimbali na kueleza kuwa hali zao zinaendelea vizuri.
“Waliofariki kwenye ajali hii wachache tumepata majina yao na wengine tunaendelea kuwatafuta ndugu zao ili waje waitambue miili maana wengi hawana utambulisho, pia kwa majeruhi wengi wameanza kujitambua,” alisema Kamanda Matei.
Juzi, Mkuu wa Oparesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi nchini, Awadh Juma Haji alitembelea eneo ilipotokea ajali hiyo na kueleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ilikuwa ni uzembe na ukaidi wa dereva wa lori.