ASKARI polisi wa Kituo cha Mrijo wilayani Chemba mkoani Dodoma, Konstebo William Werema, ameeleza alivyonusurika kifo baada ya kushambuliwa kwa mshale unaodhaniwa kuwa na sumu alipokuwa akitekeleza majukumu yake.
Muuguzi Kiongozi Wodi ya Upasuaji ya Hospitali ya Benjamin Mkapa, Sawia Arabi, akimhudumia askari polisi William Werema wa Kituo cha Polisi Mrijo, Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, aliyelazwa hospitalini hapo kwa kudaiwa kuchomwa mshale na Nanda Songo mkazi wa kijiji cha Chioli wilayani humo. PICHA: IBRAHIM JOSEPH
Werema alijeruhiwa juzi na mkazi wa kijiji cha Chioli wilayani humo, Nada Songo, baada ya kudaiwa kuwatishia makarani wa sensa kwa mishale akigoma kuhesabiwa.
Akizungumza jana katika Hospitali ya Benjamini Mkapa jijini hapo, alikolazwa kwa matibabu, askari huyo alisema alikuwa akijaribu kumkamata mtuhumiwa huyo baada ya kupokea taarifa kuwa anahatarisha amani ya wananchi wa kijiji hicho pamoja na makarani wa sensa.
“Ilikuwa Agosti 28, tulipata taarifa kwa wananchi kuwa kijijini kwao kuna mtu anatishia watu kwa mishale ikipita kwenda kwenye ng’ombe pamoja na watoto wanaopita. Sisi Jeshi la Polisi tuliokabidhiwa kulinda usalama wa raia na mali zao tulifika ili kuwasaidia wananchi hao,” alisema.
Werema alisema walipofika nyumbani kwake wakiwa wameongozana na ndugu zake, hawakumkuta mtuhumiwa na wakaelezwa kuwa anatembea na mishale.
Alisema wakiwa nje ya nyumba yake, ghafla walimwona mtuhumiwa akitoka kwenye kichaka kilicho jirani na nyumbani kwake na kumwamrisha ajisalimishe kwa amani lakini alianza kurusha mishale mfululizo na ndipo mshale mmoja ukampata tumboni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo katika kitongoji cha Manyata kijijini hapo huku akisema askari huyo alichomwa mshale unaodhaniwa kuwa wa sumu na mtuhumiwa Nanda Songo (45) ambaye alifariki dunia kutokana na kujeruhiwa na risasi maeneo ya kifuani na mguu wa kulia alizopigwa wakati akiwashambulia askari kutokana na kukaidi kukamatwa.
Pia alisema mtuhumiwa huyo alimjeruhi askari wa jeshi la akiba (mgambo) Juma Madodo kwa mshale mguu wa kulia ambaye amelazwa hospitalini kwa matibabu.
Alibainisha kuwa mtuhumiwa alikutwa na mishale 23, pinde mbili, visu viwili, ala ya kuwekea mishale, dawa mbalimbali za kienyeji na hati ya kumaliza kifungo katika gereza la King’ang’a wilayani Kondoa. Alikuwa mfungwa namba 46/2022 kuanzia Agosti 13, 2021 hadi Februari 11, mwaka huu.
ALIGOMA KUHESABIWA
Mwenyekiti wa Kijiji cha Chioli, Sadick Ndalu, alisema hakuwapo wakati wa tukio lakini alijulishwa na mtendaji wa kijiji kuwa mtuhumiwa aliwatishia kwa mishale makarani wa sensa na viongozi walipofika nyumbani kwake kutaka kumhesabu.
“Agosti 27, mwaka huu, makarani walifika lakini walipotishiwa ilitolewa taarifa ndipo polisi walipokuja hawakumkukuta na kurudi jana (juzi) wakakutana na kadhia hiyo,” alisema.
Ndalu alisema wakati askari wakimtafuta ndani ya nyumba yake alijitokeza kutoka kwenye kichaka cha jirani alipojificha na kuanza kuwashambulia askari kwa mishale.
Pia alisema mtuhumiwa aliwahi kuwashambulia watu wawili kwa mishale, kuua baadhi ya mifugo ya watu pamoja na kumshambulia kwa kisu dada yake wa kuzaliwa tumbo moja.