UJIO wa beki wa kati kutoka Burkina Faso, Mohamed Ouattara ndani ya Simba umemfanya Mkenya Joash Onyango kupigwa benchi na Kocha Zoran Maki kiasi cha kukosa mechi mbili za awali za Ligi Kuu Bara sambamba na ile ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.
Kumbe kitendo hicho cha kukalishwa benchi, kinamuuma Mkenya huyo na sasa amepanga kutuma maombi ya kutaka kuvunjwa mkataba ili asepe zake sehemu ambayo itamfanya acheze kama ilivyokuwa kabla ya ujio wa Kocha Maki na Ouattara.
Ouattara ambaye amesajiliwa kwa mapendekezo ya Zoran aliyefanya naye kazi katika klabu kadhaa ikiwamo Al Hilal ya Sudan na Wydad Casablanca ya Morocco ameingia kikosi cha kwanza akitengeneza pacha na Henock Inonga na kumng’oa Onyangoi.
Habari kutoka kwa mtu wa karibu wa Mkenya huyo zinasema huenda akapeleka maombi ya kuvunjiwa mkataba kutokana na kukosa furaha na kushindwa kupewa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza.
Onyango alipotafutwa na Mwanaspoti alisema: “Kazi yangu ni kucheza mpira haya masuala ya kimkataba nadhani yanakuwa na usiri mkubwa ndani yake ila kama kuna lolote ngoja tuone.”