Waendesha mashtaka wa Serikali nchini Rwanda, wamesema msichana mmoja Liliane Mugabekazi (24), ambaye alikamatwa kwa kuvaa mavazi yasiyo na staha anakabiliwa na kifungo cha miaka miwili jela kwa mujibu wa sheria.
Liliane ambaye alikuwa katika eneo la Burudani nchini humo, alikamatwa Agosti 7, 2022 baada ya kuhudhuria tamasha la mwanamuziki maarufu wa Ufaransa Tayc akiwa amevalia mavazi meupe yanayosadikika kukiuka taratibu na tamaduni za Taifa hilo.
“Alihudhuria tamasha hilo akiwa amevalia nguo zinazoonyesha sehemu zake za siri na ni nguo ambazo sisi tunaziita za aibu,” walisema Waendesha mashtaka hao waliokuwa wakimtuhumu kuwa kitendo hicho ni sawa na uhalifu.
Liliane Mugabekazi (24), anayetuhumiwa kuvaa mavazi yasiyo na staha mbele ya halaiki nchini Rwanda.
Wamesema, “Kwa misingi hiyo na kwa kuzingatia uzito wa tatizo tumeiomba Mahakama kumweka rumande Mugabekazi kwa siku 30, lakini pia atatumikia kifungo chake kwa mujibu wa sheria mara baada ya taratibu kukamilia.”
Hata hivyo, Msemaji wa mwendesha mashtaka, Faustin Nkusi, aliwaambia waandishi wa Hbari kuwa Mahakama itatoa hukumu Agosti 23, 2022 ikiwa atapata dhamana kwa madai kuwa kosa lake ni kushukiwa kufanya uchafu hadharani.
Aidha, Habari za kukamatwa kwake zilizua hasira miongozi mwa Wanyarwanda, lakini maafisa kadhaa wa Serikali akiwemo Waziri wa zamani wa Sheria wa Rwanda, Johnston Busingye waliunga mkono hatua hiyo.
Katika miaka ya hivi karibuni, Wanyarwanda wengi wameasi sheria kali za ukiukaji wa maadili nchini humo, ambapo mapema Machi 2022, Polisi walimkamata mwanamke mwenye umri wa miaka 20 kwa “ulevi wa umma na unyanyasaji wa aibu” baada ya video yake akiwa amelala chini katika hali ya ulevi kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Rekodi ya haki za taifa hilo la Afrika Mashariki imekosolewa vikali na wanakampeni, ambao wanaishutumu serikali ya Rais Paul Kagame kwa kukandamiza upinzani wa aina yoyote.