Bondia maarufu nchini Karim Mandonga aliyekwenda Kigoma kwa ajili ya pambano amelazimika kuahirisha safari yake ya ndege kurejea Dar es salaam leo baada ya uongozi wa Mkoa wa Kigoma kumpa dili nono la kutangaza vivutio mbalimbali vinavyopatikana Kigoma.
Mandonga amepata mwaliko wa kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Esther Mahawe na Katibu Tawa wa Mkoa huo ambapo Viongozi hao wamempongeza Bondia huyo kwa juhudi anazozionesha katika michezo yake.
Mandonga amesema anamshukuru sana Mungu kwa fursa aliyompatia ya kufahamika baada ya kupigwa na Bondia Shabani Kaoneka ambapo amesema Kaoneka ni kama amemfungulia njia ya kupata mafanikio katika maisha yake.
"Kaoneka amenipa maisha yenye msingi, kusema ukweli nilionao moyoni na sijapinga kwamba pambano lile sikupigwa na Kaonekana eti kwasababu sijui kupigana ila alinizidi ujanja akabahatisha kunipiga sehemu nyeti nikapoteza mchezo kiuhalali lakini nataka kurudiana nae ili nimuoneshe kuwa Mimi sio Mtu wa mchezomchezo, akitaka hata kesho turudiane Mimi niko tayari na wala hatonipiga tena"
"Kwa madili yangu haya ninayopata nina vitu nataka kuvipata ili kutimiza ndoto zangu, nilikuwa naishi kwenye kibanda kwahiyo natamani kupata nyumba nzuri na usafiri wa gari aina ya Jeep napigana sana kutimiza haya"