Dar es Salaam. Mbunge wa zamani wa Kilwa Kusini, Mkoa wa Lindi (CUF), Selemani Bungara maarufu Bwege ameondoka Tanzania kwenda nchini Kenya kumpigia kampeni Mgombea wa Urais wa Ushirikiano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga.
Bwege aliyepata kuwa Mgombea wa Jimbo hilo kwa tiketi ya ACT Wazalendo mwaka 2020 chama alichojiunga nacho mwaka huohuo akitokea CUF anakuwa mwanasiasa wa kwanza kutoka Tanzania kupewa heshima hiyo na Timu ya Kampeni ya Azimio la Umoja.
Kwa mujibu wa taarifa iliyolewa mapema leo Alhamisi Agosti 04, 2020 na Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma, ACT Wazalendo, Janeth Rithe imesema mvuto na hotuba tofauti alizokuwa anawasilisha akiwa bungeni ni miongoni mwa sifa zilizomfanya aitwe.
"Kumbukumbu za mtandaoni zinaonyesha kuwa hotuba za Bwege ndani na nje ya Bunge zinafuatiliwa na kupendwa sana nchini Kenya," amesema Janeth
Uchaguzi wa Kenya utafanyika Agosti 09, 2022 huku mchuano ukiwa mkali baina ya Raila na Naibu Rais William Ruto.
Hata hivyo, Tifa ambayo ni Taasisi ya Utafiti Kenya, Ijumaa ilitoa ripoti ya utafiti wake kuelekea Uchaguzi Mkuu huo na majibu ni kwamba, Odinga anakubalika kwa asilimia 46.7, wakati Ruto akiwa na asilimia 44.4.
Taasisi nyingine ya utafiti inayoitwa Centre for African Progress, nayo imechapisha ripoti yake kuwa Odinga ana uelekeo wa kushinda urais kwa asilimia 52, wakati Ruto ana asilimi 45.