CCM yampa maagizo Waziri Bashe



Tabora. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimetoa maagizo manne kwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ikwemo kumsimamisha kazi Mrajisi wa Vyama vya ushirika wa mkoa wa Tabora anayedaiwa kushindwa kutekeleza majukumu yake.

Hata hivyo, Mrajisi wa mkoa  huo, Absalom  Cheliga  alipopigiwa simu kujua ukweli wa tuhuma zinazomkabili, amedai kinachotokea kwa sasa ni msukumo wa kisiasa na kwamba madai hayo hayana ukweli wote.

"Nasajili vyama kwa kuzingatia vigezo na sheria na nimekuwa nikisimamia weledi, ninachojua kama unafanya kazi zinazogusa watu malalamiko hayakosekani na kinachoendelea sasa ni upepo wa kisiasa watu wanatumia fursa kunichafua," amesema

Kuhusu kauli ya kufukuzwa amesema, anasubiri wizara na taasisi yake iamue.


Awali, akizungumzia leo Agosti 19, 2022 na  wananchi wa Kata ya Ufuluma Wilaya ya Uyui, kuhusu suala la kufukuzwa kazi Mrajisi huyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka amesema kiongozi huyo amekuwa tatizo sugu kwa wakulima wa tumbaku mkoani hapo wanaolalamikia kuweka urasimu katika uanzishwaji wa vyama vya ushirika.

"Na amekuwa na kikundi cha mawakala anaowatumia kuwahamasisha wananchi wajiunge vikundi fulani wakati yeye si kazi yake kwa kumlazimisha mtu kujiunga na kikundi fulani," amesema

"Maelekezo yetu kwa waziri wa kilimo kumuondoa mara moja Mrajisi wa ushirika mkoa, hatutaki kuendelea kuona mtu mmoja anakwamisha juhudi za Rais kwa kuwatesa wakulima wa tumbaku," amesema

Naye Mbunge wa Tabora Kaskazini (CCM), Athuman Maige amesema kuondoka kwa kiongozi huyo wakulima wataondokana na changamoto wanazopata na kujikita kuzalisha zao ilo kwa wingi.

"Tumepamba sana kumshauri lakini hasikilizi ushauri wa viongozi na hata kwenye mkutano huu hajahudhuria anajua anayofanya akiondolewa atawasaidia," amesema

Maagizo mengine yaliyotolewa na chama hicho  kuhakikisha madeni ya wakulima wa tumbaku mkoa huo yanalipwa kabla ya msimu mpya kuanza, kusimamia bei elekezi ya mbolea ya Serikali na pembejeo na kujenga kiwanda kuchakata zao la tumbaku na kufikiria kujenga kiwanda cha sigara ili kuongeza ajira

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad