CCM yamulika Wanaojipanga Kwa Ajili ya Urais Mwaka 2025


Moshi. Wakati baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakitaka makada wenzao waendeleze utamaduni wa chama hicho wa kutochukua fomu za kuomba uteuzi wa urais ndani ya chama hicho mwaka 2025, baadhi wanataka utamaduni huo usitishwe ili kuwa na ushindani zaidi.

Licha ya hoja hiyo kutozungumzwa kwa uwazi lakini tayari kuna makundi yanayosigana juu ya jambo hilo na hivyo kuanza kutoa ishara kuwa huenda Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Hussein Mwinyi watakabiliwa na upinzani ndani ya chama wakati ukifika.

Kauli aliyoitoa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Shaka Hamdu Shaka siku chache zilizopita visiwani Zanzibar kuwa Rais Samia na Dk Mwinyi ndiyo watakaokwenda nao hadi 2030, imekoleza vuguvugu la kutaka demokrasia ya ushindani ipate nafasi.

Samuel Paul, mmoja wa makada wa CCM, aliliambia Mwananchi kuwa ni dhahiri kuwa CCM, kimefunga milango kwa makada wake wenye ndoto ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu 2025 kwa kusema Rais Samia Suluhu na Dk Husein Mwinyi watahudumu hadi 2030.

Alisema ingawa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 na ile ya CCM ya mwaka 1977 zinatambua urais ni miaka mitano mitano, lakini CCM kina utamaduni iliyojiwekea wa Rais kuhudumu kwa vipindi viwili mfululizo (miaka mitano mitano).

Vikao vya juu vya CCM kuanzia Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na mkutano mkuu kila baada ya miaka mitano hupitisha jina la mgombea wa kiti cha urais lakini utamaduni kuachiana ndio hushika hatamu.

Ni kutokana na utamaduni huo, anapojitokeza kada wa CCM kutaka kushindana na Rais aliye madarakani anayepaswa kumalizia kipindi cha pili, huonekana ni msaliti anayetaka kuvuruga chama hivyo hutakiwa kuliondoa jina lake katika mchuano.

Kada wa CCM, Benard Membe ni miongoni mwa walioonja shubiri ya kufukuzwa chama baada ya kutangaza kutaka kuomba fomu za kuwania urais kukabiliana na aliyekuwa Rais John Magufuli.

John Shibuba naye alikabiliana na joto kali la kusakamwa baada ya mwaka 2010, kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hiyo akikabiliana na Jakaya Kikwete.

Hata hivyo Shibuda hakuirejesha fomu hiyo licha ya kukamilisha taratibu zinazotakiwa ikiwemo kusaka wadhamini.

Kitendo hicho kilionekana kukaidi utamaduni wa chama hicho hivyo Shibuda, aliangushwa kwenye kura za maoni alipokuwa akiomba uteuzi wa kutetea kiti cha ubunge wa Maswa Mashariki, alichokuwa akikishikilia na hivyo kuhapia Chadema alikowania kiti hicho na kushinda ubunge.

Samson Njaidi, mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam, alisema utamaduni wa CCM unaondoa dhana nzima ya demokrasia kwa hasa kwa kuwa chama hicho ni kioo na kiongozi kwa vingine

Alisema kama Rais aliyepo madarakani akishindanishwa itaongeza umakini na chachu ya kinyang’anyiro husika.

Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wanaiona kauli ya Shaka ni ishara ya uwepo wa moto unaofukuta chini kwa chini ndani ya CCM kuelekea 2025 na wapo makada wanaojiimarisha kugombea nafasi hizo.

Kauli ya Rais Samia, aliyoitoa akiwa Ikulu Januari 4, 2022 wapo watu ambao hakuwataja majina, wanapanga safu za uongozi kuelekea 2025 na kusema ni ‘stress’ (msongo) na kutaka wasamehewe kwa kuwa wana homa ya uchaguzi.

Shaka alivyofunga mlango

Akizungumza katika kongamano la kuunga mkono jitihada za kuleta maendeleo zinazofanywa na Rais Samia lililofanyika mkoa wa Unguja Kaskazini huko Zanzibar, Shaka aliwaambia wanachama wa CCM kuwa watamalizana na Rais Samia 2030.

“Kwa kazi nzuri aliyoifanya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwaheshimisha Watanzania, ya kuheshimisha Afrika, Rais Samia tutamalizana naye 2030, penye uhai Mungu atupe uhai,” alisema Shaka katika kongamano hilo.


Msimamo huo huo akauelekeza kwa Rais wa Zanzibar, Dk Mwinyi akisema naye watamalizana naye 2030 na kusisitiza kama kuna mtu (mwana CCM) ana ndoto za kuchukua fomu 2025 kuwania nafasi hizo basi waziweke pembeni.


“Chama hiki hakijawahi kucheza bahati nasibu kweye kupata viongozi wa kuwakabidhi dhamana ya kulivusha taifa hili,” alisisitiza Shaka na kusema katika eneo ambalo chama hicho kiko makini, ni eneo la kuwapata viongozi.


Lakini kauli hii ya Shaka inaonekana kama ni mkakati mahsusi ndani ya CCM, kwani hata katika mikutano ya kiserikali, hakutakosekana kiongozi atakayemnadi Rais Samia kuelekea 2025 na hii ni kuanzia Waziri mkuu hadi mawaziri na Naibu.


Akizungumzia jambo hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe alisema aliyetoa maneno hayo ni kiongozi wa CCM na chama hicho kina katiba, miongozo na miiko ambayo haiku kwenye katiba au kanuni zake.


Alisema kitu alichokisema Shaka ni jambo linalofanyika ndani ya chama hicho kwa sababu imezoeleka Rais anapomaliza kipindi kimoja, anaachiwa kipindi cha pili ili akamilishe miaka 10 kwa mujibu wa katiba ya nchi nay a chama.


“Ukija kwenye dhana ya demokrasia, nafikiri hapo kutakuwa na maswali, kwamba demokrasia inahitaji watu washiriki kwenye uchaguzi ndani ya chama au nje ya chama. Mwisho wa siku wanaoamua hilo ni walewale ndani ya CCM ambayo of course ni demokrasia.


“Lakini ukiangalia kwenye katiba, inaelekeza kwamba kila baada ya miaka mitano, kutakuwa na uchaguzi wamchague kiongozi. Sasa wamefutaje kwenye vyama yao, wataangalia miongozo inawa-govern namna gani,” alisema Wangwe.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad