Dar es Salaam. Jiji la Dar es Salaam limetajwa kuwa jiji la pili miongoni mwa majiji 10 mazuri na yanayoendelea barani Afrika.
Baadhi ya maeneo yalitajwa kuwa ni mazuri kwa ya kupumzika ni Coco Beach na visiwa vya Mbudya.
Hayo yamebainika leo Agosti 9, 2022 wakati wa kikao kati ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla kusikiliza mikakati ya Baraza la Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) ya kulifanya jiji hilo kuwekeza katika uchumi wa buluu.
Wakati kikao hicho kikiendelea na kufika zamu ya Makalla kuzungumza, aliwaonyesha wajumbe hao video kwenye simu yake na kuwataka kuisikiliza nafasi ilipo Dar es Salaam katika majiji yaliyopo Afrika na hicho wanachotaka kwenda kukifanya.
Utafiti huo umefanywa na mtandao wa Afrika Reloaded mwaka 2021 na kuitaja Dar es Salaam kushika namba mbili ikitanguliwa na jiji la Abidjan nchini Ivory Coast.
Namba tatu imeshikwa na Addis Ababa (Ethiopia), nne ikikamatwa na Lagos (Nigeria) huku namba tano ikitajwa kuwa ni Nairobi (Kenya).
Namba sita inashikwa na Tunisia (Tunisi), saba ni Gaborone (Botswana), nane ikienda kwa Kigali (Rwanda), tisa ikishikiliwa na Windhoek (Namibia) na kumi ni Cape town (Afrika).
Baada ya hapo, Makalla alisema anashukuru Coco Beach kutajwa kuwa moja ya maeneo mazuri ya kupumzika, na kueleza kuwa maamuzi ya kuwakaribisha wabia kuwekeza ujenzi wa vibanda katika eneo hilo yalikuwa mazuri na hajutii.
“Leo jiji la Dar es Salaam linatajwa katika majiji kumi mazuri na yanayoendelea na Coco Beach kwenye mihogo kukitajwa ni eneo zuri la kupumzika,hii ni hatua nzuri na inaonyesha kuwa sikufanya kosa katika kuwakaribisha wabia kuja kuliendeleza eneo lile,” amesema Makalla.
Katika mipango hiyo ya kuendeleza fukwe ya eneo lile, Mkuu huyo wa mkoa amesema kuanzia Coco Beach hadi kufika hoteli ya Golden Tulip kuna eneo jingine lipo la heka 50 ambapo amewataka wafanyabiashara hao kulitembelea na kuona nini wanaweza kuwekeza hapo ili jiji hilo lifaidike kiuchumi na fukwe ilizojaliwa.
Wakati kwa upande wa Mbudya, Makalla amesema angependa kuona mwekezaji akijenga hoteli kule jambo litakalowaondolea adha wanaoenda kupumzika kupanda boti jioni kurejea nchi kavu na kusaidia kuongeza mapato ya jiji hilo.
Kwa upande wao TCCIA, wamesema licha ya kuwa na mipango mizuri kutaka kuwekeza kwenye uchumi wa bluu wamekuwa wakikumbana na vikwazo vingi ikiwemo kukosa vibali, utofauti wa sera kati ya sekta moja na nyingine, sheria kandamizi na kukosekana kwa wataalam katika eneo hilo.
Mwenyekiti wa baraza hilo, Vicenti Minja, amemuomba Mkuu huyo wa Mkoa kuangalia namna atakavyoweza kuwasaidia ili kuondokana na vikwazo hivyo kwa kuwa nia ya kuwekeza na kuifanya Dar es Salaam kuwa na uchumi wa bluu wanayo huku wakiahidi ushirikiano katika eneo la Coco Beacha alilitaja.