DED Malinyi aelezea siri ya mafanikio



Morogoro. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Mkoa wa Morogoro, Joanfaith Katarahiya ameeleza kuwa siri ya kufanya vizuri katika ukusanyaji mapato ni kuziba mianya yote ya utoroshaji wa mapato.

Amesema amehakikisha kila chanzo kinakusanywa na ushirikiano baina yake, watendaji wenzake na wananchi wa halmashauri hiyo ndiyo imewafanya kupiga hatua.

Joanfaith amezungumza na Mwananchi juzi ikiwa ni siku moja tangu Rais Samia Suluhu Hassan kumpongeza mkurugenzi huyo mwenye miaka 33 kwa kusimamia vyema ukusanyaji mapato.

Rais Samia alitumia sehemu ya hotuba yake juzi mara baada ya kuwaapisha wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa Ikulu jijini Dar es Salaam, kumwelezea Joanfaith aliyemteua Agosti 1 mwaka jana kufanya vizuri.


 
Katika hotuba hiyo, Rais Samia alihimiza ukusanyaji wa mapato, pia kufanya mapitio ya viwango walivyojiwekea vya ukusanyaji.

“Nina mfano, kuna halmashauri moja Morogoro huko ndani ndani, Malinyi ilikuwa inakusanya mapato kidogo sana…kale kabinti kangu kameweza.”

Katika mahojiano yake na gazeti hili kwa simu, DED huyo alisema, kila chanzo kimekuwa kikikusanywa na fedha zote zinazokusanywa zinaingia benki na hiyo ndio imewafanya kufanya vyema na hakuna upotevu wa mapato.


Alisema makadirio waliojiwekea ni kuhakikisha yanatekelezwa na fedha zinafanya yale yaliyokusudiwa.

“Malengo yangu ni kuhakikisha tunatimiza azma ya Rais kutoa huduma bora kwa kuwashirikisha wananchi kikamilifu kwenye maeneo yao,” alisema.

Kuhusu changamoto, alisema yeye ameweza kukabiliana nazo kwa kukaa mezani na madiwani kwa kuelimishana.

Kuhusu vyanzo vya mapato, alisema: “Tuna vyanzo mbalimbali, lakini chanzo kikuu na pekee ni kilimo cha mpunga.” Alisema alipoingia alikuta malengo ya Sh2.3 bilioni na mwaka jana Ni Sh2.5 bilioni.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad