DEJAN: Kama mlijua Simba imepigwa, subirini muone





‘MLETE mzunguuu!’ Ni moja ya maneno yanayoshika kasi midomoni mwa Watanzania na hasa mashabiki wa Yanga ambao wanawakejeli watani zao, Simba hasa baada ya utambulisho wa nyota mpya wa Wekundu wa Msimbazi raia wa Serbia, Dejan Georgijevic.

Yanga iliifunga Simba kwenye mchezo wa watani wa Ngao ya Jamii Agosti 13, na pamoja na tambo nyingine kauli za ‘mlete mzungu’ limekuwa maarufu zaidi.

Dejan Georgijevic ndiye ‘Mzungu’ mwenyewe na jina hilo limekuwa maarufu baada ya utambulisho wake kwenye Kilele cha Simba Day na alitambulishwa na Meneja wa habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally na kwa sasa jina hilo linaimbwa kila kona na kwenye mitandao ya kijamii.

Wakati Mzungu anapambana kuendana na maisha ya Tanzania kwenye kikosi chake kipya, Yanga wanaonekana kumbeza, ni kama wanaona wenzao wa Msimbazi wamepigwa kumsajili, kulingana na vile walivyomwona kwenye michezo miwili iliyopita, ule wa Simba Day dhidi ya St. George ya Ethiopia na dhidi ya timu yao.


Makala hii inakuletea wasifu wa Dejan ambaye ni pendekezo la Kocha Zoran Maki wote wakiwa raia wa Serbia, wapi ambako safari yake ya soka ilianzia hadi kufika Tanzania na takwimu zake kwenye kucheka na nyavu na je. Unajua kama jamaa ameonja utamu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya?

ALIKOANZIA

Dejan amelelewa kwenye misingi ya mpira kwenye timu ya vijana ya Zemun kabla ya kwenda Partizan ambayo ni moja ya klabu kubwa huko nchini kwao, Serbia.

Alikuwa hapo kwa mwaka mmoja, 2011–2012 kabla ya kurejea kwenye klabu yake ya kwanza akiwa mdogo ya Zemun, pia hiyo ndiyo sehemu aliyozaliwa mshambuliaji huyo wa Simba miaka 28 iliyopita.


Safari yake rasmi ya soka la kulipwa ilianzia hapo akitumika kwenye kikosi cha wakubwa kwenye ligi za madaraja ya chini.

Hakuwa akipata nafasi ya kutosha, aliishia kucheza michezo sita tu ya ushindani na kuamua kujiunga na Teleoptik alikopata zaidi nafasi ya kucheza.

MZOEFU BALAA

Kabla ya kutua Simba, Dejan amecheza soka la kulipwa kwenye klabu 10 tofauti, hivyo Simba ni timu yake ya 11, pia ni ya kwanza kwa Afrika.

Kati ya timu 10 ambazo amezichezea ni mbili tu ambazo alikuwa kwa mkopo, Partizan na Irtysh Pavlodar zote 2019.


Kijumla klabu alizozichezea ni Teleoptik, Spartak Subotica, Indija, Vozdovac, Ferencváros, Partizan, Irtysh Pavlodar, Velez Mostar na Domzale.

TAKWIMU ZAKE

Msimu bora zaidi kwa Dejan kwenye maisha yake ya soka barani Ulaya alikuwa akiichezea Indija msimu wa 2015–16 kwenye ligi daraja la kwanza nchini kwao ambalo ni maarufu kama Serbian First League kwenye michezo 28 alitupia mabao 14, alikuwa na wastani wa kufunga bao moja kwenye kila baada ya michezo miwili.

Tangu hapo hakuwahi kufikisha hata mabao 10 ndani ya msimu mmoja.

Msimu wa 2018/19, akiwa kwa mkopo Partizan ambayo ni moja ya klabu iliyomlea wakati akiwa mdogo, alipata nafasi ya kucheza ngazi ya juu zaidi kwenye uchezaji wake soka la kulipwa na ilikuwa Ligi Kuu Serbia ‘Serbian SuperLiga’, katika mechi tano alizocheza hakupachika bao hata moja.


Dejan aliona abadilishe upepo baada ya mambo kuwa sio na kwenda Kazakhstan kuichezea Irtysh Pavlodar kwa mkopo kwenye michezo 16 alipachika mabao mawili.

Akiwa na klabu tofauti, Serbia, Bosnia na Kazakhstan takwimu zake zinaonyesha amecheza jumla ya michezo 228 ikiwemo ligi na kupachika mabao 51.

AMEONJA UEFA MJUE

Akiwa Bosnia mwaka jana (2021), Dejan alionja utamu wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, wakati huo alikuwa akiichezea Velez Mostar.

Dejan aliichezea Velez Mostar michezo sita ambayo ilikuwa ni ya kupigania nafasi ya kwenda hatua ya makundi, chama lake lilianzia raundi ya kwanza na walipagwa dhidi ya Coleraine ya Ireland ya Kaskazini wakiwa nyumbani alicheza kwa dakika 23 wakati timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Ugenini alicheza kwa dakika 17, chama lake lilisonga mbele kwani lilishinda tena kwa mabao 2-1.


Katika raundi ya pili waliitupa nje ya mashindano, AEK Athens ya Ugiriki kwa mikwaju ya penalti 3-2 kwani mchezo wa kwanza ambao alicheza kwa dakika 21 walishinda nyumbani kwa mabao 2-1, wakiwa ugenini ambako walichapwa kwa mabao 2-1 alicheza kwa dakika 47.

Bao pakee kwenye michuano hiyo alifunga kwenye raundi ya tatu na ulikuwa mwisho wa chama lake walipokutana na Elfsborg ya Sweden kwenye mchezo wa marudiano ambao ulikuwa ugenini wakati wakitandikwa kwa mabao 4-1 mchezo wa kwanza wakiwa nyumbani walitoka sare ya bao 1-1.

AAPA KUKIWASHA

Mara baada ya mchezo wa Ngao ya Jamii kupitia ukurasa wake wa Twitter, Dejan aliandika ujumbe uliosomeka, “Licha ya kwamba nimekuwa sehemu ya familia ya Simba kwa siku chache tu, nimeumizwa na kufadhaika kwa kupoteza mechi yetu dhidi ya wapinzani wetu....”

“Kwa heshima niliyo nayo kwa mamilioni ya wafuasi wa Simba, nitateseka, nitajitahidi, nitajitolea na kufanya lolote liwezekanalo ili kutoa huduma bora kwa timu yangu, kufunga mabao na kuwafanya mashabiki wafurahi, wajivunie na daima kuwa upande wa ushindi.”

MSIKIE ULIMBOKA

Mchezaji wa zamani Simba, Ulimboka Mwakingwe anasema Dejan ni mmoja wa washambuliaji wazuri ila amecheza mechi mbili zilizokuwa na ushindani mkubwa na uhitaji wa matokeo mazuri.

“Nimeona mikimbio yake na aina yake ya kucheza ni moja ya mastraika wanaopenda kuwekewa pasi kwenye njia na kufunga kama itatokea kuna kiungo wa Simba akamjulia katika hilo atafanya vizuri,” anasema Ulimboka.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad