Dar es Salaam. Wanaume wanaofanya mazoezi ya asili ya kujenga miili ‘six pack’ huwa na mvuto kimaumbile, lakini inaelezwa kuwa zipo dawa (supplement) zinazotumika kuikuza huku zikizamisha ukuaji wa kawaida.
Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, utumiaji wa dawa hizo za ziada huleta athari kwenye homoni inayoweza kusababisha mtumiaji kupata saratani, kupoteza hamu ya tendo la ndoa, kisukari na kukosa nguvu za kiume.
Matumizi ya dawa hizo kutengeneza ‘six pack’ pia yanaweza kuwa kiini cha ugumba, madhara kwenye mishipa ya fahamu, kuota maziwa kwa wanaume na matatizo ya kisaikolojia, moyo na shinikizo la damu.
Takwimu za Wizara ya Afya za mwaka 2021 zinaonyesha kuwa, Tanzania kuna ongezeko la wagonjwa wa saratani 50,000 na inakadiriwa ifikapo mwaka 2030 kutakuwa na ongezeko la asilimia 50 ya wagonjwa wapya wa saratani.
Kauli hii ya mtaalamu inakuja wakati vijana wengi nchini wanakimbilia kwenye nyumba maalumu za mazoezi (gym) kunyanyua vyuma huku wakitumia dawa za kuongeza maumbile ili kuyajenga kuanzia kifuani hadi tumboni.
“Zile dawa ukizitumia hutakiwi kuacha mazoezi gym, halafu kuna vyakula hutakiwi kula, hasa vyenye mafuta kwa sababu dawa hizo zina vitamini fulani ambayo huenda kuongezeka kwenye misuli,” anasema Hashim Ramadhan, mkazi wa Temeke.
“Yaani mtu mwembamba kama wewe (akimaanisha mwandishi wa habari hii) ukitumia ndani ya muda mfupi unajaa, mwili unakatika katika, kwa hiyo hizo dawa zinasaidia unakuwa mkubwa sana.”
Mashuhuda
Noah Schembe, aliyewahi kuwa Mr Tanzania anasema ni kweli dawa hizo za kuongeza miili zipo na watu wanazitumia, hasa vijana.
Mr Tanzania huyo wa zamani, anasema dawa hizo zipo za aina nyingi kulingana na mahitaji ya mtu, akitaja za wenye vitambi ambazo hutumia kwa muda mfupi huku wakifanya mazoezi yanayopatikana gym.
“Hadi mtu afanikishe kuujenga mwili anatakiwa kutumia dawa hizo na chakula kwa wingi. Unaweza kutumia gharama kubwa kununua dawa na ukashindwa kupata matokeo kama huzingatii kula na zinapoisha mtumiaji huhitajika kununua nyingine,” anasema Schembe.
Muuzaji wa dawa
Theresia Silery kutoka Kampuni ya Forever Living ni mmoja wa wauaji wa dawa hizo, anasema kwa watu wenye vitambi wanatoa dawa za kuwawezesha kuwa na ‘six pack’ na ni salama kwa mtumiaji.
“Tuna bidhaa za weight loss (kupunguza uzito) na ili mtu awe na ‘six pack’ lazima akiondoe kitambi, tuna programu ya C9 ambayo ndani yake kuna dawa za kupunguza mwili, ndani ya siku tisa mtu atakuwa anatumia bidhaa zetu tano zitakazosafisha mwili huku akifanya mazoezi na kula,” anasema Dk Silery.
“Baada ya siku tisa, tuna programu ya siku 15 ambayo mtu hupunguza uzito kabisa na kupata ‘six pack’ anazozitaka na muonekano wake unakuwa mzuri.”
Akizungumzia dawa hizo kama zinafaa kwa wanawake, Theresia anasema wapo wengi wanaotumia lakini kwa wanaonyonyesha hawaruhusiwi kwa sababu dawa hizo hukausha maziwa ambayo ni muhimu kwa afya ya mtoto.
Mtaalamu JKCI atahadharisha
Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo na Utafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Pedro Pallangyo anaonya uongezaji wa mwili kwa dawa za aina zozote akisema hulazimisha ukuaji usio asili wa mwili ambao husababisha pande mbili za mwili kutokufanana ukubwa.
“Jambo la hatari zaidi ni yale maeneo yanayoongezeka seli zile haziwi na afya inayopaswa na zinakosa sifa za kuwa kwenye mwili wa binadamu, hivyo mtu anajiweka kwenye hatari ya kupata magonjwa ya misuli,” anasema Dk Pallangyo.
“Au magonjwa ya mishipa ya fahamu na damu kutokana na athari ambayo mwili haujajiandaa kusambaza damu na virutubisho kwenye hayo maeneo.”
Mbali na madhara hayo, Dk Pallangyo anasema matumizi ya kemikali hizo humuweka mhusika kwenye hatari ya kupata saratani kwa kuwa seli zinakwenda kujigawa na kuongezeka pasipo kuzingatia utaratibu wa kawaida wa mwili.
“Seli zinapata shida kwenye kuta zake, ‘chromosome’, kila kitu kwenye hizo seli kinapata dosari kubwa hivyo seli zile hupata upungufu mbalimbali.
“Sasa baada ya muda zile seli zinakwenda kuzaa seli nyingine zenye shida kubwa ambazo zote zina matatizo, hivyo dawa hizo hazina usalama, ni vizuri mtu kama anataka kuongeza sehemu ya mwili aongeze kwa njia ya asili au kufanya mazoezi,” anasema Dk Pallangyo.
“Kama unataka kuondoa tumbo, kupata ‘six pack’ au kuongeza mikono yapo mazoezi unapaswa kufanya, ni vizuri kwenye masuala yanayogusa afya ya mtu upate maelekezo kwa watu wenye utaalamu husika wakupe ushauri ambao hautakuletea madhara ya kiafya.”
Mtaalamu wa homoni anena
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani ya Kihomoni wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Mloganzila), Salama Ali anasema dawa mbalimbali zinazotumika kwa ajili ya kunenepesha misuli na kuongeza nguvu zinatengenezwa kutokana na kichocheo kiitwacho ‘Testosterone.’
“Hii ni homoni inayosaidia kutengenezeka kwa maumbile ya kiume na kupatikana kwa baadhi ya matendo ya mwanamume, ikiwamo misuli na ndevu. Utumiaji wa dawa hizi huleta madhara mengi kwa mtumiaji, ikiwamo shinikizo la juu la damu, moyo kutanuka na kiharusi,” anasema Dk Salama.
“Pia, hubadilisha mfumo mzima wa uchujaji wa damu kwenye figo na hata kuharibu ufanyaji kazi wa maini. Watumiaji wengi wa dawa hizo hutumia bila kuwa na elimu juu ya madhara yatokanayo na dawa hizo.”
Tatizo la ugumba
Dk Salama anasema wengi hukimbilia muonekano au kuongezeka kwa nguvu bila kufahamu madhara yake, huku utafiti ukionyesha watumiaji wa dawa hizo hupata ugumba kutokana na kupungua kwa uzalishaji vichocheo vya uzazi mwilini.
“Hii ni kutokana na utumiaji wa muda mrefu wa dawa hizi. Pia, hupunguza hisia za kimapenzi na kukosa uwezo wa kusimamisha uume ‘erectile dysfunction,’ anasema Dk Ali katika mahojiano maalumu na gazeti hili.
“Pia kusinyaa kwa maumbile ya mwanamume pindi anapokatisha kutumia kutokana na utumiaji wa muda mrefu na kuota maziwa kwa wanaume,” anasema Dk Salama.
“Imeonekana asilimia kubwa ya watumiaji wa dawa hizi huishia kupata msongo wa mawazo na madhara mengine ya kisaikolojia. Tafiti bado zinaendelea kuangalia faida na madhara ya dawa hizi.”
Dk Salama anasema dawa hizo pia husababisha usugu wa homoni ya insulini ambayo husaidia kushusha sukari mwilini, hivyo kusababisha mtumiaji kupata kisukari.
Unyanyuaji vyuma
Mfiziotherapia kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Alex Gowa anasema dawa zinazotumika kuongeza mwili huharibu mfumo sahihi wa ukuaji wa mwili (abnormal growth), husababisha magonjwa ya moyo, kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya saratani, matatizo ya viungo (arthritis) na athari kwenye macho.
Akizungumzia mazoezi ya unyanyuaji wa vyuma japo zipo faida, hasa za kuimarisha mgongo na misuli ya mikono, Dk Pallangyo anaonya watu wenye umri kuanzia miaka 45 wanaweza kupoteza maisha ghafla kwenye mazoezi.
“Wenye huo umri mkubwa, wanaovuta sigara, wenye uzito mkubwa na wenye historia ya shinikizo la damu, uwezekano wa kupoteza maisha ghafla wakiwa kwenye mazoezi hayo ni mkubwa,” anasema Dk Pallangyo.
“Kinachotokea, ukibeba kitu kizito unaupa moyo msongo kwa kuulazimisha usukume damu kwa kiwango kikubwa ndani ya muda mfupi ili kukidhi kukupa nguvu zaidi ya kuinua hicho kitu kizito, unaingia kwenye hatari ya kupata magonjwa au vifo vya ghafla,” anasema Dk Pallangyo.
Ushauri
Dk Pallangyo anashauri mazoezi ya unyanyuaji vyuma kama ni lazima yafanywe na watu wenye umri kuanzia miaka 20 hadi 40 kwa kuzingatia uzito wa kitu anachokibeba kama kinaendana na mwili wake.
Anaonya kubeba kitu kizito zaidi ya mwili kwa kuwa kunaongeza presha upande mmoja wa mapafu na moyo; na madhara yake ni kupoteza maisha ghafla.
Dk Pallangyo anashauri watu wenye umri kuanzia miaka 45 na kuendelea ni vyema wakafanya mazoezi ya kukimbia, kutembea, kuogelea na kuendesha baiskeli kwa kuwa hayo hayana madhara ikilinganishwa na unyanyuaji wa vyuma.