20 waliokufa kwenye ajali ya gari usiku wa kuamkia jana mkoani Shinyanga, amesimulia namna mumewe alivyomuaga ambaye jana alikuwa apokee fedha za mchezo Sh milioni 1.4.
Mume huyo, Musa Ally maarufu Weusi, ni mmoja wa watu hao 20 waliokufa katika ajali hiyo iliyotokea juzi saa 4:45 usiku katika Kijiji cha Mwakata wilayani Kahama katika Barabara Kuu ya Isaka kwenda Kahama ikihusisha magari manne.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Leonard Nyandahu alisema ajali hiyo ilihusisha magari manne likiwamo Toyota IST lenye namba ya usajili T 880 DUE lililokuwa likienda Kahama na kuligonga kwa nyuma trekta lenye namba ya usajili T 719 AUP lililokuwa limebeba kuni.
Aliyataja magari mengine kuwa ni basi dogo la abiria ‘Toyota Hiace’ lenye namba za usajili T 350 DDX lililokuwa likitoka Kahama, liligonga kwa mbele gari Scania yenye namba ya usajili T 658 DUW lililokuwa limesimama eneo la ajali.
Kamanda Nyahandu alisema watu 13 walikufa papo hapo wakiwamo watatu waliokuwa katika IST ambayo alikuwamo Weusi na dereva wa trekta alikimbia baada ya ajali hiyo.
Mariam Mussa ambaye ni mkewe Weusi, alisema jana kuwa mumewe alikuwa ni fundi wa magari katika Gereji ya Nyihogo wilayani Kahama na kabla ya kuondoka kwenda kazini alimweleza alikuwa anajisikia vibaya.
Mariam alimweleza mwandishi wa gazeti hili kuwa bibi wa marehemu alimpigia simu akaenda chumba cha maiti akiwa na wafanyakazi wenzake na alimtambua kutokana na nguo alizokuwa amevaa.
Alisema alifunga ndoa na Ally mwaka jana na wana mtoto mmoja. Mama mdogo na marehemu ambaye anafanya kazi Mfuko wa Hifadhi wa NSSF wilayani Kahama, Kaisiki Majid alisema mama mzazi wa Ally alifariki dunia akamuacha Ally akiwa mdogo, akamlea na kumsomesha hadi alipofunga ndoa mwaka jana.
Mfanyakazi mwenzake na Ally, Vicent Jackson alisema kijana huyo aliondoka gereji kwenda kutengeneza gari aina ya Scania eneo la Isaka.
“Leo hii (jana) marehemu ilikuwa zamu yake ya kupokea mchezo kiasi cha shilingi milioni 1.4, lakini hajarudi kuja kuzipokea,” alisema Jackson anayefanya kazi gereji moja na Ally.
Aliongeza: “Niliposikia kuwa kuna ajali, sikujua kama angekuwemo na yeye tulipata taarifa kuwa alikuwa anarudi Kahama majira ya saa nne baada ya kumaliza kazi Isaka.”
Majeruhi aliyelazwa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Paul Sebastian (35) aliyekuwa kwenye Toyota Hiace, alisema aliona gari ndogo aina ya Toyota IST likigonga lori baada ya kuipita Toyota Hiace.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk Deogratias Nyanga alisema walipokea miili 17 ya watu waliokufa kwenye eneo la ajali, majeruhi watatu walipoteza maisha wakati wakipata tiba hospitalini hapo na wengine 15 walikuwa wakipatiwa matibabu.
Dk Nyanga alisema wanawake watatu na wanaume 17 wamepoteza maisha kwenye ajali hiyo. Majeruhi mwingine, Daines Haule (43) amevunjika mkono wa kulia na mapaja yote na anatarajiwa kupewa rufaa Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga au Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza.
Dk Nyanga aliwataja majeruhi wengine kuwa ni Paul Sebastian (44), Omary Shabani (26), Kulwa Omary (27), Mahubi Tembo (29), Joseph Tumaini (37), Ally Emmanuel (18), Paschal Joseph (32), Saimon John (40), Hamis George (29), Henry Haule (37), Mwasiti Samwel (39) na Salim Slimu (37).
Mbunge wa Kahama Mjini, Jumanne Kishimba jana alitoa Sh milioni moja kwa ajili ya dawa za kutibu majeruhi hao.
Katika salamu zake kutokana na ajali hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan amevitaka vyombo vinavyosimamia usalama barabarani kuongeza juhudi za kudhibiti ajali na akawapa pole wafiwa na akaungana na familia za waathirika katika kipindi hiki kigumu cha majo