Haruna Niyonzima Aikataa Simba "Wanayokazi Kubwa Sana Kurejesha Makombe Mbele ya Aziz K na Mayele"


KIUNGO aliyewahi kutamba na Yanga pamoja na Simba, Haruna Niyonzima amekiri kuziona kiundani timu hizo mbili msimu huu, lakini akaweka wazi kwamba Simba bado itakuwa na wakati mgumu wa kurejesha mataji yake mbele ya Yanga hii ya kina Mayele na Aziz Ki.

Niyonzima ambaye kwa sasa yupo Tanzania na timu yake ya Taifa ya Rwanda, alisema kwa kikosi ilichonacho Yanga kwa sasa anaona kabisa ina asilimia 80 ya kubeba ndoo mbele ya watani wao hao - Simba pamoja na Azam FC iliyoonekana kujengwa upya msimu huu.

Haruna aliyewika na Yanga kuanzia 2011 hadi 2020 na kuhamia Msimbazi ambako hata hivyo hakudumu kabla ya kurudi Yanga, alisema timu zote zimefanya usajili mzuri, lakini Yanga ina nafasi kubwa na imeonyesha hilo wazi kwenye Ngao ya Jamii.

Ameeleza ni kama Yanga imeendelea ilipoishia kwani msimu uliopita ilikuwa na kiwango bora na kikosi imara na msimu huu imeongeza wachezaji bora ambao wataisaidia tofauti na Simba aliyesema ni kama inaanza upya.

“Timu zote zina vikosi bora. Simba misimu miwili nyuma ikiwemo kipindi nilipokuwa pale ilikuwa bora zaidi ya Yanga na kila mmoja aliiona kutokana na watu waliokuwepo na ilivyocheza.

Yanga msimu uliopita ilifanya mapinduzi kwa kuweka pesa na kusajili wachezaji bora ambao waliungana na kuwa kitu imara kisha kuipiku simba,” alisema Niyonzima ambaye wakati anaitwa Yanga akitokea APR alifahamika kama Fabregas.

Aidha nyota huyo anayesifika kwa kupiga pasi za uhakika, chenga na kuongoza timu alipoulizwa anauona wapi ubingwa wa msimu huu, moja kwa moja aliipa Yanga asilimia 80 za kubeba kombe tofauti na timu nyingine ikiwemo Simba.

“Yanga ya msimu huu imejipanga sana, imeweza kubakisha mastaa wake wote wa msimu uliopita na kuongeza wengine bora hivyo itasumbua sana na kwa nilivyoiona ligi hadi sasa ni ngumu kuizuia Yanga kuwa Bingwa,” alisema.

Alizungumzia dili lake la kurejea kukiwasha bongo ambapo alihusishwa kujiunga na Singida Big Stars na Geita Gold na kuweka wazi kuwa; “Ni kweli timu zaidi ya mbili zilinitafuta zikitaka huduma yangu lakini hatukuweza kufikia makubaliano kutokana na maslahi binafsi.”

Ujue mpira ndio unaendesha maisha na faimilia yangu, asilimia kubwa ya mali nilizonazo zote zimetokana na mpira hivyo lazima niuheshimu na kuwa na mipaka ya maslahi nadhani hiyo ndio sababu kuu ya dili hizo kutokamilika,” alisema supastaa huyo na kuongeza kuwa hajachuja kiwango kutokana na nidhamu, malengo na kujituma kwake mazoezini na uwanjani. Sasa anakipiga timu ya AS Kigali ya Rwanda, pia ni nahodha wa Rwanda (Amavubi) ambayo jana ilikuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa kuvaana na Ethiopia iliyoomba mechi za nyumbani kupigwa Kwa Mkapa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad