Hassan Mwakinyo Auota Mkanda wa WBO 'Nasubiria Siku Nitakayo Tangazwa Kuwa Bingwa"



Bondia Hassan Mwakinyo amesema kwa Morari aliyonayo katika Mazoezi ya kuelekea Pambano lake la Kimataifa anatamani kutwaa mkanda wa Dunia wa WBO.


Mwakinyo anatarajiwa kupanda ulingoni Septemba 03 mwaka huu kupambana na Liam Smith wa England katika Jiji la Liverpool.


Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Mwakinyo ameandika namna anavyopata Morari akiufikiria mkanda huo anaokwenda kuusaka siku hiyo.


“Mara kadhaa naijiwa na Morari sana kila nikitafakari juu ya usiku ambao nitatangazwa kuwa Bingwa wa WBO rasmi kutoka Makorora Tanga Tanzania” ameandika Mwakinyo


Bondia huyo aliyehamishia makazi yake kwa muda hadi nchini Marekani amekua akijifua katika mazoezi ya nguvu kuhakikisha anatimiza ndoto zake za kuwa Bingwa wa Dunia wa WBO.


Kupitia ukurasa wake wa Instagram amekua akiweka Picha zinazoonyesha namna anavyofanya mazoezi ya nguvu kiasi cha kupata vidonda kwenye vidole, ikionyesha wazi anajipanga vyema kwenda kuipeperusha vizuri Bendera ya Tanzania.


Mwakinyo mwenye nyota tatu na nusu atambana na Liam Smith mwenye nyota nne ambaye ni mzoefu akiwa amecheza Mapambano mengi 35, na kati ya hayo ameshinda Mapambano 31, akipoteza matatu na kupata sare katika Pambano moja.


Kwa upande wa Mwakinyo amecheza Mapambano 22, kati ya hayo ameshinda Mapambano 20 na kupoteza mawili. Kati ya 20 aliyoshinda, 14 ameshinda kwa KO na TKO.


Iwapo Mwakinyo atashinda Septamba 03, atazidi kupanda katika viwango vya Ubora Kimataifa, na itakua ni mara ya pili anapigana na Bondia kutoka England, baada ya mwaka 2018 kumpiga Sam Eggington katika Pambano lililounguma mjini Birmingham.


Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad