HISIA ZANGU: Mandonga amepigwa lakini anabakia kuwa mshindi



 
MOJA ya vitu vilivyonogesha katika pambano lililoitwa Thriller in Manila kati ya Muhammad Ali na Joe Frazier ‘Smoking Joe’ ni namna ambavyo Ali alivyotua katika Jiji la Manila nchini Philippine siku chache kabla ya pambano akiwa na kinyago alichokifananisha na Frazier.

Akatembea nacho mitaani huku akikipiga makonde akikifananisha na mpinzani wake. ilikuwa ni kejeli iliyompandisha hasira Frazier huku ikiwaacha watu wakiwa na hamu kubwa ya kutazama pambano hilo. Lilikuwa moja kati ya pambano bora zaidi la ngumi kuwahi kutokea duniani.

Hii pia ilikuwa tabia ya Ali katika mapambano mengi. Alikuwa na mdomo mchafu dhidi ya wapinzani wake ndani na ulingo wa ngumi. Mwaka 1974 pale Kinshasa wakati akipigana na George Foreman alikuwa akisikika anamwambia “Haya rusha hizo ngumi zako mtoto wa kike.”

Hiki ndicho ambacho amenifurahisha mtu anayeitwa Karim Mandonga. Tofauti yake na Ali ni kwamba Mandonga sio mbabe katika ngumi. Ni mbabe katika mdomo tu. Pambano la pili mfululizo anapigwa vibaya na mpinzani wake lakini Mandonga ameisimamisha nchi.


 
Katika wikiendi ambayo Man City walikuwa wanacheza na Liverpool, huku Alphonce Simbu akiwa mshindi wa pili wa Marathon katika michezo ya Madola, habari ya mjini ilikuwa Mandonga. Hatukusikia habari za Simba na Yanga isipokuwa za Mandonga tu. Amefanya tusahau kila kitu na kuamua kushughulika naye.

Mpaka sasa habari ya mjini ni Mandonga. Ngumi zinataka hivi. Michezo inataka hivi. Pengine Mandonga alipaswa kulipwa na Azam Media pesa nyingi zaidi kwa sababu pambano lake limetazamwa na watu wengi zaidi pengine kuliko pambano lolote la ngumu mwaka huu nchini Tanzania.

Mandonga (pichani) amefanya promosheni. Inawezekana yeye alipigwa lakini kwa upande mwingine Mandonga ni mshindi. Kwa upande mwingine mchezo wa ngumi uliibuka kuwa na ushindi mwingi katika wikiendi hii iliyoisha.


Nilikuwa mahala Sinza nikitazama pambano la Manchester City dhidi ya Liverpool. Mara tu pambano lilipomalizika mashabiki walilipuka wakitaka mhudumu ahamishe idhaa na kuweka pambano la Mandonga. Hata mashabiki wa Liverpool ambao timu yao ilikuwa imeshinda hawakutaka kuona nahodha wao, Jordan Henderson akikabidhiwa ngao. Hamu yao ilikuwa kutazama pambano la Mandonga.

Katika soka kuna matukio mengi ya kusisimua ya kila siku. Lakini pia mchezo wenyewe umekuwa maarufu kwa sababu misingi yake. karibu kila mtu anashiriki akiwa mtoto. Lakini baadaye pia kuna matukio mengi ambayo yanaufanya mchezo kuwa maarufu.

Kwa sasa waanze kusifiwa Azam TV kwa kurudisha msisimko wa ngumi kwa sababu tunatazama mara kwa mara. Lakini hapo hapo mabondia wanahitaji kujipromoti wenyewe kama Mandonga alivyofanya. Inaongeza msisimko.

Ni kama ilivyo katika muziki. Wanamuziki wanajipigia promosheni kwa kuongea mambo mengi ya kujisifu. Inaleta ushindani mkubwa baina yao. Katika ngumi mastaa walipaswa kuwa kama Mandonga. Hauwezi kuwa bondia bora lakini usiye na maneno ya shombo.


 
Maneno ya ovyo ndio ladha ya mchezo wenyewe. Mandonga huwa hamtukani mtu. Haongei lugha chafu isipokuwa anatoa vitisho vingi kwa adui. Bahati mbaya kwake, au tuseme bahati mbaya kwa mchezo wa ngumi Mandonga huwa anapigwa.

Kwa kusisimua kama alivyofanya, ni rahisi kwa Mandonga kupata biashara nyingine nje ya mchezo wake. Ni rahisi kufanya matangazo. Amejitengenezea mvuto wa kipekee. Kampuni zitaanza kumsaka kwa ajili ya kutangaza bidhaa zao. Nani hatataka kufuatana na Mandonga katika safari yake ya maisha mema?

Lakini pia ni rahisi kupata dili jingine la kupigana kwa sababu watu wanataka kumuona akipigana. Pambano lake linaweza lisiwe kuu lakini bado akawa anapata dili za matangazo ya utangulizi. Ni kama alivyolifunika pambano kuu kati ya Suleiman Kidunda na Erick Katompa.

Kinachonishangaza kwa Mandonga ni namna ambavyo ameibuka uzeeni katika mchezo huu. Naambiwa ana umri wa miaka 43 na amecheza mechi sita tu. Alikuwa wapi? ni kitu kinachoshangaza. Inawezekana anapigika kwa sababu ameingia katika mchezo uzeeni.

Anaonekana anaupenda mchezo wenyewe lakini umri umemtupa mkono. Lakini angeingia katika mchezo akiwa kijana mdogo si ajabu leo angekuwa mbali. Pambano lake la hivi karibuni alilodundwa na Maghambo Christopher, Mandonga alionekana akiwa hana mbinu za kuficha sura yake vema.

Pambano la majuzi limemuonyesha Mandonga hana pumzi ya kutosha. Kinachosikitisha ni umri wake sidhani kama ataweza kupata pumzi ya kutosha siku za usoni. Ameingia katika mchezo akiwa katika umri wa kustaafu.

Pamoja na udhaifu wake lakini ameusimamisha mchezo wa ngumi wikiendi hii iliyoisha. Ameupa hadhi. Mchezo wa ngumi ni mchezo wa nyodo. Ni mchezo wa mbwembwe. Ni mchezo ambao ni tofauti na soka ambapo wachezaji huwa hawajisifu sana isipokuwa wamewaachia mashabiki.

Huku katika ngumi unaanza kujisifu mwenyewe kwanza. Ni kama ambavyo Hassan Mwakinyo naye ambavyo pia amejitahidi kujipromoti kwa kujionyesha yupo tofauti na mabondia wengine kwa kila kitu. Ndondi na muziki wa Hip Pop vinakwenda sambamba. Haishangazi kuona mara nyingi mabondia huwa wanasindikizwa ukumbini na marafiki zao ambao ni wanamuziki wa Hip Pop. Hongera tena kwa Mandonga. Ni kweli amepigwa lakini ukitazama jinsi ambavyo alivyofanikiwa kujiweka katika midomo ya watu basi ni wazi yeye amebakia kuwa mshindi. Mandonga amesababisha pia tumjue hata na mpinzani wake, Shaban Kaoneka ambaye wengine tusiofuatiliua ngumi kwa karibu tulikuwa hatumfahamu. Ni wazi kuanzia sasa tutaanza kumfuatilia kwa karibu. Hii yote ni kwa sababu ya Mandonga.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad