JICHO LA MWEWE: Onyango anajiuliza maswali ambayo hata sisi tunajiuliza



UVUMI ni mwingi kuhusu Joash Onyango. Kwamba anataka kuondoka zake Msimbazi na kutokomea kwingineko baada ya Kocha wa Simba, Zoran Maki kumuacha akilipasha moto benchi la timu hiyo. Unaweza kusadiki uvumi huo ni wa kweli kwa sababu Onyango hakuzoea hivyo.

Hadi sasa Joash itakuwa hajui ni kitu gani kimempiga usoni. Itakuwa ni kitu kizito chenye ncha kali. Kwa misimu yote amekuwa beki wa kati namba moja. Ametengeneza kombinesheni na Kennedy Juma. Halafu akadumu muda mrefu na Sergi Wawa Paschal.

Alipoingia Mcongo mwenye makeke, Enock Inonga ilibidi Wawa aanze kusugua benchi huku Onyango akicheza sambamba na Inonga. Maisha yalikuwa mazuri kwake. Haikuwa bahati mbaya Onyango aliendelea kuwa beki namba moja wa Simba.

Watu wa Yanga walijaribu kumvunja nguvu Onyango kwa kumuita Mzee. Mara kadhaa niliwauliza ni mzee gani anayeweza kuwa na kasi kama ya Onyango? Mzee gani anayeweza kuusoma mchezo kwa umakini mkubwa na kulihami lango lake?


Ni mzee gani anayeweza kuwadhibiti washambuliaji wa timu pinzani juu na chini? Hata katika pambano ambalo Inonga alimsindikiza nje ya uwanja Fiston Mayele alikuwa ni Onyango ndiye aliyemdhibiti vilivyo Mayele lakini Inonga akaenda kujichukulia sifa za bure mbele ya kamera za Azam TV kwa kumsindikiza nje Mayele alipokuwa akitolewa.

Lakini ghafla amekuja beki anayeitwa Mohammed Ouattara. Beki wa kimataifa wa Burkina Faso. Haikujulikana kama beki huyo amekuja nchini kwa ajili ya kuwa msaidizi wa Onyango na Inonga, au amekuja nchini kwa ajili ya kuanza kucheza moja kwa moja na kuchukua nafasi moja ya Onyango au Inonga.

Na sasa tumejua kwamba kumbe alikuja nchini kuchukua nafasi ya Onyango. Nilichopenda kutoka kwa Kocha wa Simba, Zoran Maki ni kwamba hakutaka kuwa mnafiki. Hakutaka kubadili mfumo wake kwa ajili ya kumridhisha beki wa tatu wa kimataifa katika kikosi chake.

Hakutaka kwenda katika mfumo wa kutumia mabeki watatu kwa ajili ya kuwaridhisha mabeki wake watatu wa kimataifa kutoka Congo, Kenya na Burkina Faso. Ameamua kwenda na Inonga na Ouattara. Hii ina maana imegharimu nafasi ya mmoja kati ya wachezaji muhimu katika historia ya Simba miaka ya karibuni.

Kitakachokuwa kinamshangaza Onyango ni kile kile ambacho kinatushangaza sisi. Ametupwa nje huku kiwango chake kikiwa kile kile ambacho tunakifahamu. Ametupwa nje ya kikosi bila ya kufanya makosa uwanjani. Labda alifanya makosa katika mechi za kirafiki za Misri ambazo hatukuziona wakati Simba ilipokuwa infanya maandalizi ya msimu mpya.

Vinginevyo katika macho ya wengi ukiwauliza mashabiki wa soka bila ya kujali itikadi zao, ni beki gani bora kati ya Onyango na Inonga nadhani wengi watakwambia ni Onyango. Ingawa hachezi na jukwaa lakini amekuwa na sifa nyingi zaidi uwanjani kutokana na uimara wake.

Kama hali ikiendelea hivi basi Onyango atakuwa na maswali mengi kichwani. Lini nafasi yake itakuja? Januari mwakani anatimiza miaka 30. Wachezaji wa umri wake huwa hawapendi kukaa benchi. Ukimtazama katika benchi unamuona wazi hana furaha. Hii ni tabia ya kishindani ambayo wanayo wanasoka wengi wa kimataifa kasoro wanasoka wa Tanzania.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad