JPM Magufuli Daraja la Sita Afrika




Muonekano wa baadhi ya nguzo kati ya nguzo 22 zilizoinuliwa katika mradi wa ujenzi wa daraja la JP MAGUFULI Kigongo/Busisi jijini Mwanza. Daraja hilo litakuwa na jumla ya nguzo 67 hadi kukamilika kwake, litakuwa na urefu wa Kilometa 3.2 na upana Mita 28.45.

Imeelezwa kuwa Daraja la JP Magufuli, linalojengwa jijini Mwanza litakalo ziunganisha wilaya za Misungwi na Sengerema kupitia Ziwa Victoria linatarajiwa kuwa daraja refu kuliko yote Afrika Mashariki na Kati na litakuwa la sita kwa urefu katika Bara la Afrika kwa takwimu za sasa.

Hayo yamesemwa jijini Mwanza na Joseph Haule ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara (Road Fund Board), wakati wajumbe wa Bodi hiyo wakikagua utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa daraja hilo.

“Kama mnavyoona Tanzania sasa tunazidi kupaa, tumeona madaraja mengine mengi makubwa na mazuri yakichukua rekodi lakini sasa daraja hili ndilo litakalovunja rekodi nchini, Africa Mashariki na Kati, na kwa kweli mradi huu utakapokamilika tutajivunia sisi watanzania”


Kazi za usukaji wa nondo zikiendelea katika mradi wa ujenzi wa Daraja la JP Magufuli, Kigongo/Busisi jijini Mwanza.
Ameyataja madaraja marefu zaidi Afrika kwa takwimu za sasa kuwa ni Daraja la 6th October lililopo nchini Misri lenye urefu wa km 20.5, Daraja la Third Mainland nchini Nigeria km 11.8, Daraja la Suez Canal nchini Misri km 3.9, Daraja la Kisiwa cha Msumbiji km 3.8, pamoja na Daraja la Dona Ana nchini Msumbiji km 3.67.


 
“Tumeambiwa kwamba itakapofika 2024 daraja hili litakabidhiwa kwa Serikali kama ilivyo kwenye mkataba wa ujenzi wake, licha ya changamoto za Uviko 19, maji kuongezeka, pamoja na uwepo wa miamba chini ya maji. Inafurahisha zaidi kwamba vifaa kama nondo na simenti zinazotumika katika mradi huu zinatoka hapa nchini” amesema Haule.

Ameongeza kuwa Bodi ya Mfuko wa Barabara imetembelea mradi wa ujenzi wa daraja la JP Magufuli kwa kuwa Bodi ndiyo itakayokuwa na dhamana ya kuhakikisha kwamba daraja hilo linatunzwa wakati wote na kwamba Bodi imeridhika na teknolojia inayotumika katika ujenzi huo.


Mhandisi Mshauri wa mradi wa ujenzi wa Daraja la JP MAGUFULI kutoka kampuni Yooshin Engineering Corporation, Mhandisi Abdulkarim Majuto akifafanua jambo kwa wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wakati wakikagua mradi huo jijini Mwanza.
Naye Mhandisi Mshauri wa mradi huo kutoka kampuni ya Yooshin Engineering Corporation, Mhandisi Abdulkarim Majuto, ameeleza kuwa kasi ya utelelezaji wa mradi ni nzuri na kwamba hadi sasa mradi umefikia asilimia 48.9, ambapo jumla ya nguzo 22 kati ya 67 zimeshainuliwa na tayari wameanza kulaza beam na baada ya hapo zoezi litakalofuata ni kumwaga zege na hatimaye kuweka lami.


Akiongelea gharama za mradi, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Mwanza, Mhandisi Paschal Ambrose ameiambia Bodi kuwa ujenzi wa daraja la JP Magufuli unagharimu jumla ya shilingi za Kitanzania bilioni 716.3 na kwamba unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia mia moja. Hadi kufikia mwezi Julai mwaka huu, tayari Mkandarasi ameshalipwa shilingi bilioni 223 na Mhandisi Mshauri ameshalipwa shilingi bilioni 3.29. Aidha jumla ya shilingi bilioni 3.1 zimelipwa kama fidia kwa jumla ya waathirika 165 waliopisha mradi huo.

Faida za Mradi Lameck Masunga ambae ni mkazi wa eneo la Busisi wilayani Sengerema, amewaambia waandishi wa habari kuwa ujenzi wa Daraja la JP Magufuli umeleta neema kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo kwani watu wengi hasa vijana wameweza kupata ajira mbali mbali katika mradi huo wenye jumla ya ajira 764 kwa wazawa, kati ya ajira zote 820, lakini pia biashara za usafirishaji kwa kutumia bodaboda zimeimarika kwa kuwa kuna idadi kubwa ya watu wanaoingia na kutoka kwenye eneo la mradi.

Kwa upande wake Esta Jumanne ambae pia ni mkazi wa Busisi, ameishukuru Serikali kwa utekelezaji wa mradi huo, kwani utakapo kamilika utaondoa adha kubwa ya kusubiria kivuko kwa ajili ya kuvuka kwenda upande wa Misungwi, ambapo kwa sasa inawachukua zaidi ya saa moja kuvuka kwenda upande wa pili wakati kwa kutumia daraja itakuwa ni chini ya dakika tano.

Awali, Mhandisi Rashid Kalimbaga ambae ni Meneja Msaidizi (Ufundi), kutoka Bodi ya Mfuko wa Barabara, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, kazi ya Bodi ya Mfuko wa Barabara ni kukusanya fedha kwa ajili ya matengenezo ya barabara zote Tanzania bara pamoja na madaraja yake, ili kuhakikisha kuwa madaraja na barabara zote nchini zinakuwa kwenye ubora wake kwa vipindi vyote vilivyokadiriwa.


 
Daraja la JP Magufuli litakapo kamilika, litaziunganisha wilaya za Misungwi na Sengerema ambazo zimetenganishwa na Ziwa Victoria katika barabara kuu ya Usagara kupitia Sengerema hadi Geita. Barabara hiyo pia ni sehemu ya barabara zilizoko kwenye Ushoroba wa Ziwa Victoria ambayo inaanzia Sirari mpakani na Kenya hadi Mutukula mpakani na Uganda (792.5km).



Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad