Kenya: IEBC yabadili Kauli ‘Ruto Hakuongezewa Kura’

 


Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeibuka hadharani tena na kudai kuwa mgombea urais wa muungano wa Kenya Kwanza William Ruto hakuongezwa kura elfu kumi kama inavyodaiwa na wengi.


Awali, iliripotiwa kuwa Naibu Rais William Ruto alikuwa ameongezewa kimakosa kura elfu kumi katika eneo la bunge la Kiambu mjini na kura hizo kuondolewa mara moja baada ya kosa hilo kutambulika.


IEBC, kupitia kwa afisa wake Kamishna Justus Nyangaya, imesisitiza kuwa hakuna mgombea yeyote wa urais ambaye aliongezewa kura zisizokuwa zake.


“Waliandika 14,760 katika fomu B. Na katika fomu C ilibadibilishwa na kurejesha kuwa 14,860. Ruto William ana 41,050. Hakuna mahali ambapo tuliongeza 10,000 kwa mgombea yeyote. Natumai hili limeeleweka na litarekebishwa. Asante,” Nyangaya alisema.


Kwa mujibu wa ripoti ya IEBC, Ruto alikuwa ameorodheshwa kupata kura 51,050 katika eneo bunge la Kiambu katika Fomu 34B badala ya 41050.


Ni kosa ambalo lilitambuliwa wakati wa kujumuishwa kwa kura na likarekebishwa mara moja. Hali ya kujumuisha kura inaendelea katika ukumbi huo wa Bomas ambapo wakala wa Azimio na Kenya Kwanza waweka umakini.


Wakati huo huo, Mgombea urais wa UDA William Ruto amewataka Wakenya kumuamini Mungu, huku wakisubiri matokeo ya urais.


Ruto alisema ni jukumu la kila mtu kupiga kura, ila Mungu ndiye muamuzi wa mwisho kuhusu ni nani atakayechukua hatamu za uongozi nchini.


Akizungumza wakati wa ibada ya kanisa nyumbani kwake Karen jumapili ya Agosti 14, iliyohudhuriwa na watu wake wa karibu kisiasa, Ruto alisema tayari Mungu amekwishaamua ni nani atakayekuwa rais wa tano wa Kenya.


Wakati huo huo, aliwahimiza Wakenya wawe na subira huku Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka, IEBC ikiendelea kuhakiki kura za urais.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad