Kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja Kwanza nchini Kenya, Raila Odinga amewaambia Viongozi wa Dini kuwa wamekusanya ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba uchaguzi wa Agosti 9 ulikuwa na mkanganyiko.
Odinga, ameyasema hayo mara baada ya kukutana na Viongozi hao wa dini Agosti 20, 2022 na kudai kuwa kuwa, uamuzi wa mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Wafula Chebukati kumtangaza Dkt Ruto kuwa rais mteule umeigawa nchi.
“Muungano wa Azimio tayari umekusanya ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba tamko lililotolewa na Chebukati na mchakato uliotumiwa kufikia uamuzi huo ni wa uwongo na unaichafua nchi ndani na nje ya bara la hili.
Kiongozi wa Azimio la Umoja Kwanza, Raila Odinga akiwa na Viongozi wa Dini nchini Kenya. Picha na NMG.
Amesema, kumtangaza Ruto kuwa rais mteule bila kufuata utaratibu, IEBC haikuwa tu imekiuka haki ya kidemokrasia ya mamilioni ya Wakenya waliopiga kura katika uchaguzi wa Agosti 9, bali pia imefichua nchi kudhihakiwa kikanda na kimataifa.
Aidha, amesema uamuzi wa kuhamia kortini una lengo la kusaidia kujenga na kurejesha nafasi ya kidemokrasia nchini Kenya, ambayo ipo katika hatari ya kuchafuliwa na maamuzi yaliyogawanyika na IEBC kwa kumsafisha Dkt Ruto.
“Tayari tunaona wengine wakijiita rais mteule ilhali tunajua kwamba uamuzi wa IEBC haukuwa wa wingi wa makamishna hao saba, kwani waligawanyika wanne wanapinga kitendo cha mwenyekiti na watatu wanaunga sasa hapo nani mkweli,” alihoji Odinga.
Ameendelea kubainisha kuwa, “Tumesema tunataka kuona haki kwa sababu hapo ndipo tutakuwa na amani ya kudumu na kama vile marehemu Askofu Mkuu Desmond Tutu alivyosema, bila ukweli na haki na amani, kamwe hakuwezi kuwa na maridhiano.”
Kiongozi huyo wa ODM, amesema matamshi tofauti yaliyotolewa na Chebukati na mpishano wa kauli za makamishna wanne waliopinga IEBC ni ushahidi tosha kwamba shughuli ya uchaguzi ilitatizwa.
“Inaonekana IEBC, wanapishana kauli na hakuna anayeonekana kujua kilichotokea na ikiwa waliopewa jukumu la kusimamia uchaguzi wanaweza kutuletea aibu hii, basi ina maana kwamba demokrasia yetu ingali changa,” ameongeza Odinga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, Askofu Mkuu Martin Kivuva ambaye aliongoza msafara wa Makasisi kufika nyumbani kwa Odinga, amesema ziara hiyo ilikuwa maalum kwa kufanya maombi na Odinga mara baada ya kuisha kwa uchaguzi.
Katika msafara huo, Askofu huyo mkuu aliandamana na Viongozi wengine wa kidini akiwemo Mkuu wa Kanisa la Kianglikana la Kenya, Jackson ole Sapit na alisema uamuzi wa Odinga kuhamia kortini ni njia bora zaidi kwake ya kutafuta amani.
“Tunafuraha na kutiwa moyo kuwa Odinga ana hamu ya kuona kwamba amani inaendelea kuwepo hata tunapotafuta njia za kuamua ni nini hasa kilifanyika na kupata kujua ukweli,” alisema Askofu Mkuu Kivuva.