Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ambaye alikuwa akimpigia debe Raila Odinga wakati wa kampeni, ameonekana hadharani tena na kuondoa ukimya uliokuwa umetanda dhidi yake kufuatia IEBC kumtangaza mrithi wake, William Ruto.
Kenyatta, amevunja ukimya huo baada ya ugeni wa Seneta Chris Coons wa Marekani, ambaye walifanya naye mazungumzo katika Ikulu ya Nairobi, ambaye awali kiabla ya kukutana na Kenyatta, Croose alifanya mazungumzo na Ruto.
Amesema, “Kenya itasalia kuwa thabiti katika kusisitiza maadili ya utawala bora ili kuhakikisha kwamba nchi inahifadhi hadhi yake kama mfano mzuri wa demokrasia katika bara hili kwa kuhakikisha amani katika kipindi hiki cha mpito inaimarika.”
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta. Picha kwa Hisani.
Rais huyo pia alisema, lengo lake kuu ni kuona amani itashinda na kwamba Wakenya kwa pamoja wanaweza kuweka mfano katika bara la Afrika na ulimwengu mzima kwa kuendeleza mshikamano baina yao.
Makatibu wa Baraza la Mawaziri, Raychelle Omamo na Betty Maina, pamoja na Balozi wa Marekani nchini Kenya Meg Whitman, walikuwa miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo.