Nairobi. Msimamizi wa uchaguzi wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya kwenye jimbo la Gichugu, Geoffrey Gitobu amefariki dunia jana Jumatatu Agosti 22, 2022 baada ya kuanguka ghafla.
Meneja wa Uchaguzi wa IEBC kaunti ya Kirinyaga, Jane Gitonga amethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kusema uchunguzi wa mwili wa marehemu utafanywa ili kubaini chanzo cha kifo cha ofisa huyo.
Hata hivyo, mmoja wa maofisa wa IEBC ambaye hakutaka jina lake kutajwa amesema kuwa Gitobu alizidiwa ghafla akiwa anaendesha gari barabarani.
"Alikuwa akiendesha gari mjini alianza kujisikia vibaya na akatafuta msaada wa huduma kwenye zahanati ya mtu binafsi lakini baadae gari la wagonjwa lilimchukua na kumkimbiza Hospitali ya Cottage ambako alifariki kabla ya kuhudumiwa,”kimesema chanzo hicho.
Tukio hilo linatokea saa chache tangu, mgombea urais wa tiketi ya Azimio la Umoja, Raila Odinga na mgombea mwenza wake, Martha Karua wafungue kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 9, 2022 kwenye mahakama ya juu ya Milimani.
Moja ya madai yao ni kukaguliwa kwa fomu namba 34A za matokeo ya urais ambazo zinasainiwa na wakuu wa vituo.
Katika uchaguzi huo, mgombea wa Kenya Kwanza, William Ruto aliibuka mshindi kwa kupata kura milioni 7.1 akimshinda mpinzani wake Odinga aliyepata kura milioni 6.9.