Kocha Nabi aitolea uvivu Bodi ya Ligi, TFF




Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Nasreddine Nabi ameiangushia lawama Bodi ya Ligi ‘TPLB’ pamoja na Shirikisho la soka Tanzania ‘TFF’ kwa kushindwa kufuata misingi na taratibu za muda wa kuanza kwa Msimu Mpya wa Ligi Kuu.

Kocha huyo kutoka Tunisia anaamini Muda wa Kuanza kwa Ligi umekua mchache baada ya kumalizika kwa msimu wa 2021/22, huku baadhi ya Wachezaji wake wakiitwa katika majukumu ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa Bingwa Afrika ‘CHAN’.

Amesema asilimia kubwa ya Wachezaji wake wamekosa muda mzuri wa kupumzika baada ya kumaliza mchezo wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ dhidi ya Coastal Union ya Tanga uliochezwa Jumamosi (Julai 02), baada ya kutakiwa kurudi kambini haraka kuanza maandalizi ya msimu ujao.

“Jambo linalonisumbua ni ratiba ya Bodi ya Ligi TFF, kwa kawaida Duniani kote inatakiwa baada ya msimu wachezaji uwape siku 20 za mapumziko ambapo hawatafanya jambo jingine zaidi ya mapumziko, hawatakiwi kabisa kuwaza mambo ya mpira kwa wakati huo.”


“Baada ya hapo timu inatakiwa ipate preseason ya wiki sita, lakini ukiangalia ratiba ya TFF, kuanzia mechi ya mwisho ya Kombe la Shirikisho, Julai 2, 2022 mpaka mechi ya Ngao ya jamii ni wiki sita tu, utafanya mazoezi siku ngapi na likizo itakuwa siku ngapi?”

“Tunaomba TFF ifanye mpangilio vizuri wa likizo na kuipa timu muda mzuri wa maandalizi, hii itasaidia hata wachezaji wa ndani, mfano Tanzania kuna wachezaji wazuri kama Feisal na Dickson Job, hawajapata muda mzuri wa kupumzika sababu walikuwa timu yaTaifa, TFF wangebadilisha tarehe ya kuanza ligi, itasaidia hata timu nyingine, sio Young Africans pekee,” amesema Nabi.

Young Africans itacheza mchezo wa kuwania Ngao ya Jamii Jumamosi (Agosti 13) dhidi ya Simba SC, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.


Kabla ya mchezo huo Young Africans itacheza dhidi ya Mabingwa wa Soka nchini Uganda Vipres SC, Mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki katika kilele cha Wiki ya Wananchi, Jumamosi (Agosti 06), Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad