LICHA ya Yanga kumuongezea mkataba kocha wao, Nasreddine Nabi wa miaka miwili lakini inatajwa kuwa mkataba huo una masharti mazito matatu ambayo kama akishindwa kuyafikia basi muda wowote panga litamkuta.
Yanga usiku wa kuamkia jana Ijumaa ilitangaza kumuongezea Nabi mkataba mwingine wa miaka miwili baada ya ule wa awali kumalizika mwishoni mwa msimu huu ambao mpya utamalizika 2024.
Awali kocha huyo alikuwa akitajwa kutimkia klabu za Wydad Casablanca na FAR Rabat zote za nchini Morocco mara baada ya kumtangazia ofa nono.
Mmoja wa mabosi wa Yanga, ameliambia Championi Jumamosi kuwa, haikuwa rahisi rahisi kwao kufanikisha mipango ya kumbakisha kocha huyo mwenye rekodi nzuri msimu uliopita.
Bosi huyo alitaja masharti ambayo amepewa kocha huyo ni: “Sharti la kwanza ambalo kubwa alilopewa Nabi ni kuhakikisha anatetea makombe yote matatu waliyoyachukua msimu huu.
“La pili, ni kuivusha na kuifikisha na kuivusha katika hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa msimu huu “La tatu, ni kulichukua Kombe la Mapinduzi ambalo limechukuliwa na Simba, na kama akishindwa moja wapo yatakuwepo mazungumzo na kama akishindwa yote, basi safari itawadia kwake kuondoka Yanga,” alisema bosi huyo na kuongeza kuwa:
“Nabi amekubaliana na masharti hayo ambayo yatambakisha hapo kwa mafanikio makubwa katika msimu huu na kuahidi kutimiza hayo yote yaliyokuwepo katika mkataba huo mpya.”
Nabi alizungumzia hilo kwa kusema: “Ilikuwa ngumu kwangu kuondoka Yanga kwa hivi sasa, kwani bado nina mipango mikubwa ndani ya timu ambayo ninatakiwa kuikamilisha msimu huu.