MAAFISA nane wa tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini Kenya (IEBC) wamekamatwa na Polisi na kusimamishwa kazi baada ya kukutwa wakifanya mkutano wa siri.
Maafisa hao wamekamatwa katika kaunti za Homabay, Kisumu na Bungoma ambapo walikutwa wakiwa na baadhi ya wagombea wa nafasi tofauti katika Uchaguzi Mkuu unaofanyika leo Agosti 9, 2022.
Maafisa wengine wanne wa tume hiyo ya uchaguzi wamesimamishwa kazi katika maeneo ya Bunge ambayo ni Ndiwa na Webuye Mashariki mwa nchi hiyo.
Maafisa hao wamesimamishwa baada ya kukutwa wakiwa wamekutana kwa siri na wagombea wa kiti cha wawakilishi wa Bunge la kaunti moja nchini humo na wagombea wa Ubunge.
Kwa mujibu wa ushahidi wa video uliotolewa na Polisi unaonyesha kwamba katika mojawapo ya tukio alionekana Naibu Msimamizi wa kituo cha kupigia kura akimshawishi mkubwa wake kukubali kwa lengo la kumsaidia mmoja wa wagombea kupata ushindi.
Baadhi ya maafisa wengine wa tume ya uchaguzi katika kaunti ya Bungoma wametoroka baada ya wenzao kukamatwa nyumbani kwa mmoja wa wagombea.
Hayo yamejiri baada ya wananchi kutoa taarifa kwenye kituo cha Polisi huku ikibainika kwamba mshukiwa aliyekamatwa amewekwa chini ya ulinzi katika kituo cha Polisi cha Webuye.