Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Leonard Nyandahu
KUFUATIA ajali iliyopoteza maisha ya watu 20 wilayani Kahama, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Leonard Nyandahu, ametaja majina ya baadhi ya watu waliofariki dunia. Anaripoti Paul Kayanda, Kahama … (endelea).
Nyandahu amewataja waliopoteza maisha katika ajali hiyo na kutambuliwa na ndugu kuwa ni pamoja na Jonas Kija Mkazi wa Wilaya ya Kishapu, Paul Cheo mkazi wa Wilaya ya Kishapu, Tungu Magege Mkazi wa Wilaya ya Kishapu, Salinja Bukelonge, Siti Ngoseka (46), Nuhu Mpinga(28) mkazi wa Nyihogo Wilaya ya Kahama.
Wengine ni Agustino Mnyamba(28) Kanu Lutema Mkazi wa Kata ya Mwakata Wilayani Kahama, Leonard Basu na Musa Daud Mkazi wa mtaa wa Bukondamoyo Manispaa ya Kahama.
Ajali hiyo imetokea usiku wa jana Jumatatu saa 4.00 usiku eneo la kata ya Mwakata Halmashauri ya Msalala chanzo cha ajili hiyo kikiajwa kuwa uzembe wa madereva wote wa magari yaliyohusika.
Kamanda huyo amefafanua kuwa kulitokea ajali mbili tofauti, ajali ya kwanza ilihusisha Trekta iliyokuwa imesimama pembezoni mwa barabara bila kuwepo kwa kiashiria chochote kinachonyesha kusimama hali ambayo ilisibabisha gari ndogo aina ya Toyota IST kuligonga kwa nyuma na kusababisha majeruhi.
Aidha amesema kuwa ajili ya pili ilihusisha gari aina ya Toyota Hiace iliyokuwa ikitokea Wilayani Kahama ikielekea Tinde Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga iligongana uso kwa uso na Lori wakati likijaribu kukwepa ajali iliyotokea awali baina ya IST na Trekta.
Kufuatia hali hiyo kamanda Nyandahu,ametoa wito kwa madereva wote kuwa wawapo barabarani wahakikishe wanachukua tahadhari ikiwa nipamoja na kuzingatia sheria za usalama barabarani kwani matukio mengi yamekuwa yakitokea kwa uzembe wa madereva hao.
“Nawaonya madereva wote wasiozingatia sheria za usalama barabarani kwa sasa sheria itachukua mkondo wake ikiwemo kuwafutia leseni, na kwa tukio hili kila mmoja ajilinde niwaambie tu kwamba jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga halitacheka na dereva yoyote kuanzia sasa,”amesema kamanda Nyandahu.