MAKABILIANO makali baina ya makundi mawili pinzani ndani ya IEBC yanatarajiwa katika Mahakama ya Juu baada ya kuwasilisha kortini nyaraka za kupakana tope Jumamosi.
Nyaraka za viapo zilizopelekwa Mahakama ya Juu zimedhihirisha mgawanyiko mkubwa kati ya kundi linaloongozwa na mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati na lile la makamishna wanne linaloongozwa na Naibu Mwenyekiti Juliana Cherera.
Kundi la Bi Cherera ambalo pia linajumuisha makamishna Justus Nyang’aya, Francis Wanderi na Irene Masit, linadai Bw Chebukati alishirikiana na watu kutoka nje, ambao hawakuwa wafanyakazi wa IEBC kubadilisha matokeo ya urais ili kumfaa Rais Mteule William Ruto.
Kwa mara ya kwanza, IEBC inaenda kortini ikiwa imegawanyika – makamishna watatu –Bw Chebukati, Profesa Abdi Guliye na Boya Molu – wanaunga mkono ushindi wa Dkt Ruto huku wanne wakipinga na kumshambulia Bw Chebukati.
Aidha, itakuwa mara ya kwanza kwa Mkuu wa Sheria kujitenga na IEBC katika kesi ya kupinga matokeo.
Bw Nyang’aya alifichua kuwa raia wa kigeni, Gudino Omor, ambaye hakuwa mfanyakazi wa IEBC, alitumiwa na Bw Chebukati kuondoa kwenye mitambo ya IEBC fomu halali za 34A zilizokuwa zikitumwa kutoka vituo vya kupigia kote nchini na kupakia fomu feki.
Kulingana na Bw Nyang’aya, Omor alianza kuvuruga sava za IEBC kuanzia Juni 1, mwaka huu, na aliendelea hadi baada ya Uchaguzi.
Alifichua kuwa, watu wengine 377 wa kutiliwa shaka waliingia katika mtambo wa sava na kuvuruga sava.
“Kufikia sasa, Bw Chebukati hajawahi kutupatia taarifa kuhusiana na watu hao 377,” anasema Bw Nyang’aya katika kiapo hicho alichokula mbele ya mawakili wa Rachier & Amollo Advocates.
Bw Nyang’aya alifichua kuwa, alipokonywa na Bw Chebukati majukumu ya kusimamia mitambo ya matokeo na kuagizwa kupokea wageni waliokuwa wakiingia katika ukumbi wa Bomas.
Kwa upande wake, Bi Cherera alidai mwenyekiti wa IEBC alikuwa anakarabati matokeo kutoka katika maeneobunge akiwa mafichoni na kisha kuwapa makamishna kwenda kusoma mbele ya wanahabari katika Bomas.
Makamishna Bi Cherera, Bw Nyang’aya, Bw Wanderi na Bi Irene Masit walijitenga na matokeo yaliyotangazwa na Bw Chebukati ambapo Dkt Ruto aliibuka mshindi wa urais.
Bi Cherera katika ushahidi wake anadai Bw Chebukati alijitengenezea matokeo akiwa mafichoni na kisha kuwalazimisha makamishna wenzake kuyakubali.
“Tuliondoka Bomas na kuelekea katika Hoteli ya Serena ambapo tulitangaza kukataa matokeo,” akasema Bi Cherera.
Mwanasheria Mkuu Paul Kihara Kariuki jana Jumamosi aliwasilisha barua katika Mahakama ya Juu akisema hana nia ya kupinga kesi ya Bw Odinga dhidi ya IEBC.
IEBC imekodisha kampuni 26 za kisheria kutetea ushindi wa Dkt Ruto. Kati ya kampuni hizo, 10 zitatetea Chebukati ambaye pia ameshtakiwa na mlalamishi Bw Raila Odinga na mwaniaji mwenza wake Martha Karua wa Azimio la Umoja One Kenya.
Naibu wa Rais, William Ruto anatetewa na mawakili 54 katika kesi hiyo ambayo itaanza kusikilizwa Jumanne.
Idadi ya mawakili wanaowakilisha Bw Odinga na Bi Karua ilifikia 44 jana baada ya kuongeza mawakili wawili – Dkt Otiende Amollo na Bw Donald Kipkorir.
Naye, Bw Chebukati katika stakabadhi zake alizopeleka mahakamani jana alijitetea vikali huku akisema uchaguzi ulikuwa huru na haki.
Alidai Baraza Kuu la Usalama wa Kitaifa (NSAC) lilikuwa limemuonya dhidi ya kumtangaza Dkt Ruto mshindi wa urais kwa kigezo kuwa machafuko yangetokea nchini.
Alidai Katibu wa Masuala ya Utawala katika afisi ya Rais Kennedy Kihara, Inspekta Jenerali Hillary Mutyambai, Naibu Mkuu wa Jeshi Francis Ogola na Wakili wa Serikali Kennedy Ogeto walienda Bomas alfajiri na kujaribu kumshawishi kubadili matokeo.
Bw Chebukati pia anasema wandani wa Bw Odinga, akiwemo aliyekuwa Seneta wa Busia Amos Wako, walienda kumuahidi mabilioni ya fedha endapo angetangaza kinara huyo wa Azimio mshindi wa urais.