Makamishna Wanne wa IEBC Waliokataa Matokeo Kenya Ngoma Ngumu Kwa Ruto Mahakani


MPIRA mgumu ambao Dk William Ruto (President Elect) anapaswa kuucheza ni kushawishi (kama inawezekana), au kumwomba Mungu, Makamishna Wanne wa IEBC waliokataa matokeo yaliyompa ushindi, wabadili mawazo. Wakubali kuzungumza lugha moja na Chairman Wafula Chebukati.

Vinginevyo; Makamishna Wanne waliopinga matokeo, wakiendelea na msimamo wao. Kisha wakatokea mahakamani kutoa ushahidi dhidi ya uamuzi wa mwisho wa IEBC uliompa ushindi Ruto, Mahakama Kuu Kenya itakuwa na kazi ndogo mno kufanya uamuzi.

Hoja za kuwa Tinga Raila Odinga aliibiwa kura au Azimio la Umoja kulalamikia mchakato kukosa uwazi. Kesi za jinai za Naibu Rais Mteule, Rigathi Gachagua, ambazo nazo ni hoja nzito mahakamani. Yote hayo ni masuala ambayo bila shaka Majaji watashughulika nayo kivyao.

Ninachokijengea hoja hapa ni kipengele cha wazi kabisa ambacho kipo kisheria. Ni Makamishna wanne kati ya saba wa IEBC kuyakataa matokeo na kulalamika kukosekana uwazi kwenye majumuisho ya mwisho ya kura.


Sheria No 9 ya 2011 Kenya (Independent Electoral and Boundaries Commission Act), ukurasa wa 21, kipengele namba 7, inaelekeza kuwa uamuzi wa IEBC utakuwa wa muundo wa wengi wape.

Sasa, Wanne wamegoma. Watatu wamemtangaza Ruto kuwa mshindi. Wengi ni wanne. Watatu ni wachache. Hivyo, wachache ndio wamemtangaza Ruto mshindi kinyume na maelekezo ya Sheria No 9 ya 2011.

SWALI

Mwaka 2017, Wafula Chebukati alimtangaza Uhuru Kenyatta kuwa mshindi wa urais na matokeo yakapinduliwa na Mahakama Kuu. Uchaguzi ukarudiwa.

Ikitokea mwaka huu tena, Mahakama Kuu ikapindua matokeo, Chebukati atakuwa mgeni wa nani?

USHAURI

Team Hustlers endeleeni kusherehekea kwa matumaini.

Team Baba endeleeni kungoja sarakasi za mahakamani kwa matumaini.

Ngoma mbichi hii

Ndimi Luqman MALOTO
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad