Mapya ofisa TRC aliyefukuzwa kazi kwa kupinga tozo




Dar es Salaam.  mbalimbali wametoa maoni tofauti kuhusu kufukuzwa kazi kwa Meneja wa Shirika la Reli nchini (TRC) Kanda ya Dar es Salaam, Jonas Afumwisye huku baadhi yao wakionyesha nia ya kumpatia msaada wa kisheria.

Juzi, Afumwisye alipokea barua iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa ikimjulisha uamuzi wa shirika hilo wa kumfukuza kazi kutokana na kile alichoeleza kuwa ni kuthibitishwa kwa makosa aliyoyafanya mwaka jana.

Baadhi ya makosa anayotuhumiwa kuyafanya ni kupinga juhudi za Serikali za kuanzisha tozo kwenye miamala ya simu na pia kupinga chanjo inayotolewa kwa wananchi kwa ajili ya magonjwa ya milipuko.

Kadogosa alibainisha makosa mengine kwenye barua hiyo kuwa ni kukashifu viongozi wakuu wa nchi, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson kupitia makundi ya kijamii.


Wakizungumza na Mwananchi kuhusu kufukuzwa kwa mfanyakazi huyo, mawakili mbalimbali wamesema wako tayari kumsaidia Afumwisye kwa sababu hajatendewa haki katika kufukuzwa kwake na wengine wamebainisha kwamba alikiuka kanuni za utumishi wa umma.

Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa alisema yuko tayari kumtetea kijana huyo kupitia taasisi yake kwa sababu ana uhuru wa kutoa maoni yake.

“Sio fair (haki) kabisa, tena mwambie kabisa, mimi binafsi ninajitolea kumsaidia kumtetea kupitia sehemu yangu, kwenye vyombo vya kisheria. Yeye ni kama Watanzania wengine kama sisi na wengine wengi ambao wanahoji hizo tozo,” alisema Olengurumwa.


Wakili kiongozi kutoka kampuni ya Haki Kwanza, Alloyce Komba, alisema atakuwa tayari kumsaidia endapo atajua kesi yake ilitokana na nini, lakini kama ilitokana na tamko la Mkurugenzi Mkuu wa TRC, basi ataweza kusaidia.

“Sisi wanasheria tunasema hapana, ni unfair termination (amefukuzwa isivyo halali) ambayo haujafanyiwa judicial process (taratibu za kimahakama) kwa sababu tunasema hata mtu aliyeua dhahiri, lazima ufuate taratibu,” alisema Komba.

Aliongeza kwamba kuna taratibu za kumfukuza mtumishi wa umma, ikiwa ni pamoja na kumsikiliza, kumwonya na kisha kuchukua hatua kama aliyopewa ya kufukuzwa kabisa katika ajira yake.

Komba alisisitiza kwamba kwa nafasi yake kama mtumishi wa umma, jambo lake limepewa uzito na kwamba katika utumishi wa umma, kosa la kutotii mamlaka linatazamwa kwa jicho kali zaidi kuliko makosa mengine.


“Kwa hiyo, maoni yangu ni kwamba administratively (kiutawala), kuna hayo masuala ya insubordination (kutotii mamlaka), lakini legally (kisheria) ningependa kujua kama utaratibu wa kisheria ulifanyika,” alisema Komba.

Kwa upande wake, wakili wa kujitegemea, Jebra Kambole, alisema watu wana uhuru wa kujieleza na kutoa maoni na kwamba hilo siyo sababu ya kumfukuza kazi ili mradi kazi zake anazifanya kikamilifu.

Alisema hata mtu aliyeko serikalini ana haki ya kutoa maoni na hadhani kama kufanya hivyo kunaweza kuchukuliwa kama kitendo cha utovu wa nidhamu kiasi cha mwajiri wake kumfukuza kazi.

“Mimi namshauri akate rufaa kwa sababu uamuzi huo unakiuka Katiba na sheria za nchi. Katiba haijasema watumishi wa umma hawana uhuru wa kutoa maoni, imesema kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni,” alisema Kambole.

Alisisitiza kwamba Afumwisye ana haki ya kukata rufaa na kusikilizwa na kwa mazingira ya kufukuzwa kwake, anaweza kupatiwa msaada wa kisheria endapo mamlaka za awali zitaamua vinginevyo.

Mwasisi mwenza wa kampuni ya uwakili ya FMD Legal Consultants and Advocates, Onesmo Mpenzile alisema kosa kubwa ambalo linasimamiwa kwa ukali na Serikali ni kutotii mamlaka.

Alisema Ofisi ya Rais ndiyo inaongoza utumishi wa umma, hivyo mtumishi yeyote wa umma anatakiwa kuheshimu mamlaka za juu yake kwa sababu sheria, kanuni na utaratibu katika utumishi wa umma unaelekeza hivyo.

Juzi Afumwisye aliliambia Mwananchi kuwa anafanya utaratibu wa kukata rufaa ndani ya siku 45.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad