Mapya yaibuka waliouawa wakawekwa kwenye viroba




MKUU wa Mkoa wa Tanga, Omari Mgumba, amesema miili ya watu wawili kati ya watatu waliookotwa katika kitongoji cha Dibabara, Kijiji cha Kwastemba wilayani Kilindi, inadhaniwa kuwa ni ya wauzaji wa madini waliouawa eneo lingine na kutupwa hapo.

Miili hiyo iliyookotwa Agosti 11, mwaka huu, ikiwa imewekwa kwenye mifuko ya sandarusi na kusafirishwa na gari ikatupwa na watu wasiojulikana kisha watu hao kuondoka.

Kutokana na tukio hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni, ameelezea kusikitishwa na mauaji hayo na kusema uchunguzi wa kina unaendelea kufanyika ili kuwabaini waliohusika na kitendo hicho.

Masauni, aliyasema hayo jana alipotembelea chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali Teule ya Wilaya ya Kilindi ya Songe, inayomilikiwa na  Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, akiwa ameambatana na kamati ya ulinzi na usalama baada ya habari ya tukio hilo kuripotiwa na gazeti la Nipashe Agosti 17, mwaka huu.

"Tumesikitishwa na tukio hili la kinyama. Tumeshuhudi  maiti na tumepata maelezo kutoka kwa madaktari na vyombo vyetu vya usalama. Japokuwa ni mapema mno kusema, nitoe wito kwa Jeshi la Polisi kuendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini waliohusika na tukio hili la kinyama dhidi ya raia wenzetu," alisema.


"Jambo hili halikubaliki kwa namna yoyote ile. Si utamaduni wala desturi yetu na hata katika mazingira ambayo wametekeleza matukio haya ni jambo ambalo tutawaeleza wananchi kwamba serikali inalichukulia kwa uzito mkubwa, na tutafanya kila linalowezekana tuhakikishe vyombo vyetu vya usalama vinawatia mikononi wahusika," alisisitiza.

Masauni pia, alibainisha kwamba jambo hilo linaonyesha kuwa  kuna uwezekano wa kuwapo kwa hali ya uhalifu, ujambazi au watu wanaotumia majambazi katika kutekeleza uhalifu huo na wa aina nyingine.

"Lakini kwa namna yoyote ile uchunguzi ndio utakaotuwezesha kujua ukweli. Cha  muhimu zaidi ni kuhakikisha wale waliofanya uhalifu huu wanapatikana mara moja na sheria kuchukua mkondo wake," alisema.


Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba, alisema tukio hilo limeleta taharuki mkoani hapa na nchini kwa ujumla kwa kuwa limesababisha watu kushindwa kuendelea na shughuli zao na kwenda kutambua miili ili kujiridhisha kama ni ndugu zao.

"Lakini tukio kama hili limeuchafua mkoa wetu na taifa letu kwa sababu uhalifu huu ni kama uhalifu mwingine. Kwa hiyo nataka niwahakikishie Tanga itaendelea kuwa salama na majeshi yetu yote ya ulinzi na usalama yatafanya jitihada," alisema Mgumba.

Alifafanua kwamba, kwa uchunguzi wa awali unaonyesha tukio la mauaji hayo halikufanyikia mkoani Tanga isipokuwa wauaji walikwenda kuitupa miili hiyo wilayani Kilindi.

"Ukiangalia zile picha watu walipakia kwenye viroba vya kilo 50 lakini wamekunja kama vya kilo 20. Inaonekana  ni watu wazoefu kwa mauaji," alisema.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Safia Jongo, alisema: "Tumepokea kwa masikitiko tukio hili lakini, tulishaanza kufanya uchunguzi. Pia makao makuu ya polisi yameshaunda timu itakayokuja kushirikiana na sisi kufanya uchunguzi wa kina ili kuwapata wahalifu."

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad